Nyota Namungo walioachwa Angola kurejea Jumatatu

Muktasari:

Awali nyota hao walitarajiwa kurudi leo, lakini kutokana na taratibu za kodi imepelekea kutoondoka mpaka jumatatu

HATIMAYE wachezaji wa timu ya Namungo waliosalia Nchini Angola wanatarajiwa kurejea Machi Mosi baada ya kubainika kupona ugonjwa wa Covid 19.

Takribani wiki mbili sasa, wachezaji wa wawakilishi hao katika michuano ya Kimataifa ya kombe la Shirikisho walikumbana na sintofahamu wakiwa uwanja wa ndege nchini humo iliyopelekea mchezo wao na Primeiro Agosto kutochezwa.

Nyota hao watatu ni Lucas Kikoti, Fred Tangalu pamoja na Khamis Faki akiwemo pia Mtendaji Mkuu wa klabu ya hiyo Omary Kaaya .

Mwenyekiti wa Namungo Hassan Zidadu ameiambia Mwanaspoti leo kuwa, wameishafanya mipango ya kuwarejesha nyota hao ambapo walitarajia kurudi leo lakini kutokana na sababu za ulipaji kodi walizokuwa wakishughulikia haitawezekana.

"Tayari tushafanya kila kitu ili wenzetu waweze kurudi Tanzania, na wangekuja leo lakini kuna masuala ya ulipaji kodi Nchini humo yamekwamisha ujio huo leo, ila jumatatu watarejea,"

"Maana Angola kuna ndege mbili tu, Jumamosi na Jumatatu pekee zaidi ya hapo hakuna, tunamshukuru sana Mungu ndugu zetu wako salama kabisa,"amesema.

Wakati huo huo Zidadu amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana kuwaondosha Agosto katika mchezo wa mtoano kwa jumla ya mabao 7-5 na kutinga hatua ya makundi ya kombe hilo.

"Tumeingia hatua ngumu ambayo inahitaji kupambana ili kufanya vizuri, mpaka tulipofika sasa tunamshukuru sana Mungu na wachezaji wetu wamepambana vilivyo wasichoke huku mbele ni kugumu zaidi,"