Ni Simba vs Azam fainali

Mabao mawili yaliyofunga na Meddie Kagere na Pape Sakho yameivusha Simba hatua ya fainali ya Kombe la Mapinduzi ambapo sasa watakutana na Azam FC.

Kagere alifunga bao hilo dakika ya 15 huku Sakho akifunga dakika ya 48 dhidi ya Namungo mechi iliyomalizika Simba ikishinda bao 2-0 Uwanja wa Amaan kisiwani hapa.

Azam wao wametinga hatua hiyo wakiwaondoa mabingwa watetezi Yanga kwa penalti 9-8 baada ya suluhu ya bila kufungana dakika ya 90 hivyo kuyaaga rasmi mashindano hayo.

Katika mchezo huo Simba ilionyesha kudhamiria kutinga fainali kutokana na namna ambavyo wachezaji wao walivyokuwa wakipambana kulishambulia lango la wapinzani huku wapinzani wenyewe wakifika langoni kwa kushitukiza.

Namungo chini ya kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' kipindi cha kwanza walionekana kuzuia zaidi kuliko kushambulia ingawa walibadilika kidogo kipindi cha pili kwa kujaribu kushambulia.

Sakho alionekana kuwakamata zaidi Namungo kwani mashambulizi yake mengi yalifika kwa wapinzani huku akiwa na kasi kubwa ya kuwapita wapinzani wake.

Sakho ndiye aliyeibuka pia mchezaji bora wa mecho hiyo akipewa Sh1 milioni na wadhamini wao huku mchezaji wa Namungo Frank Magingi akizawadiwa Sh 300,000 kwa kuwa mchezaji mwenye nidhamu ya mchezo (fair play)