Nabi ataja sababu ya Morrison kuanzia benchi

Muktasari:

  • Nabi amesema anatamani kumtumia Morrison kwa muda zaidi pengine kuliko mtu yoyote lakini kutopenda mazoezi makali zaidi ndio kitu kinachomkwamisha kumpa muda mrefu zaidi.

Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amevunja ukimya juu ya matumizi ya winga Bernard Morrison akisema Mghana huyo hana pumzi ya kutosha kucheza muda mrefu uwanjani.

Nabi amesema anatamani kumtumia Morrison kwa muda zaidi pengine kuliko mtu yoyote lakini kutopenda mazoezi makali zaidi ndio kitu kinachomkwamisha kumpa muda mrefu zaidi.

"Watu wengi wanataka kumuona Morrison anacheza lakini sisi makocha ndio tunajua ubora wa kila mchezaji kwa kila dakika kuanzia mazoezini mpaka uwanja wa mchezo,"amesema Nabi.

"Morrison wa Sasa ni vigumu kumpa muda zaidi ya huu tunaompa labda abadalike kwa kujiweka tayari zaidi, ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana ndio maana tulimleta hapa lakini kwasasa hayuko tayari kucheza kwa muda mrefu zaidi ya huu tunaompa watu waelewe hili,"amesema Nabi

"Hakuna kocha ambaye ataamua kumweka nje Morrison kwa kipaji chake kama yuko sawasawa, watu wasidhani sisi makocha hatupendi kuona timu inashinda Mimi sio kocha wa kumpa nafasi mchezaji kwa jina lake au presha ya nje ya uwanja tofauti na kile anachonionyesha uwanja wa mazoezi.

Aidha Nabi ameongeza kuwa kikosi chake kitakachocheza kesho kwenye mchezo wa pili wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji wao USM Alger anaamini kutakuwa na ubora mkubwa wa kuipigania timu hiyo.

Yanga inahitaji ushindi wa mabao 2-0 na kuendelea kuweza kupindua matokeo na kuchukua ubingwa baada ya kulala nyumbani kwa mabao 2-1 wiki iliyopita.