Mwadui waikazia Yanga dakika 45

KIPINDI cha kwanza cha mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Mwadui kimemalizika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kwa sare ya bao 1-1.

Mchezo ulianza kwa kasi, huku timu zote mbili zikishambuliana kwa kupokezana.

Dakika ya saba Mwadui walipata bao la kuongoza kupitia kwa Aniceth Revocatus aliyefunga kwa kichwa.

Dakika ya 21, Yanga walisawazisha bao hilo kupitia kwa Bakari Mwamnyeto aliyefunga kwa kichwa akimalizia mpira wa faulo uliopigwa na Said Ntibanzonkiza.

Baada ya bao hilo, lango la Mwadui liliendelea kushambuliwa kwa kasi huku Ntibanzonkiza na Feisal wakikosa baadhi ya mabao ya wazi.

Dakika ya 34, Ntibanzonkiza aliwatoka mabeki wa Mwadui na kupiga Kiki ya chini chini iliyompita kipa Mussa Mbise na kugonga mwamba.

Ntibanzonkiza aliendelea kuwasumbua mabeki na viungo wa Mwadui huku wakimkaba kwa nguvu na dakika ya 36 Walace Kiango alionesha kadi ya njano baada ya kumchezea rafu.

Zikiwa zimesalia dakika tatu kutamatika kwa dakika 45 za kipindi cha Kwanza, Yanga walipata penati haada ya beki wa amwadui Mgeveke Jorum kumchezea rafu Feisal Salum ndani ya Boksi penati iliyopigwa na Fiston AbdulRazack na kupanguliwa na kipa Mbise.