Muda mtamu hapa, afichua ishu ya simu

Muktasari:

  • Mudathir amekuwa kwenye kiwango cha juu kwenye michezo kadhaa iliyopita, huku akifunga mabao yaliyoipa ushindi timu yake kwenye michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara ya hivi karibuni.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameeleza juu ya kiwango kizuri cha kiungo, Mudathir Yahya huku akikiri ana faida kubwa uwanjani, lakini mabao yake yakafichua jamaa anavyojua kumaliza mechi akiwa anacheza eneo la juu.


Mudathir amekuwa kwenye kiwango cha juu kwenye michezo kadhaa iliyopita, huku akifunga mabao yaliyoipa ushindi timu yake kwenye michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara ya hivi karibuni.


Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema Mudathir ni mchezaji anayefiti kwenye nafasi tatu tofauti uwanjani na zote amekuwa akimpa matokeo mazuri akimpanga.


“Mudathir licha ya kufunga pia ni kiungo ambaye anaweza kukaba, kutengeneza mashambulizi na kufunga, hivyo ni mzuri akicheza namba sita, nane na 10;


“Nafurahishwa na namna anavyocheza na ni mchezaji msikivu, ukimwelekeza nini cha kufanya uwanjani anafanya hivyo hivyo, suala la kuanza au kuanzia benchi hilo ni jukumu langu,” alisema kocha huyo raia wa Argentina.


Kauli hiyo ya Gamondi inakuja wakati ambao Mudathir ameifungia timu yake mabao sita kwenye mechi za ligi, lakini matano kati ya hayo akiyafunga akiwa amepewa majukumu ya kucheza kama kiungo mshambuliaji nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.


Utamu ni, Mudathir amekuwa akibadilisha nafasi na kucheza na akili kwa kukaa eneo ambalo anamalizia kwa utulivu akiwa eneo la hatari la wapinzani.


Yanga vs KMC 5-0
Bao pekee alilolifunga Mudathir akiwa nje ya eneo la hatari ni dhidi ya KMC, mzunguko wa kwanza, Yanga ikishinda mabao 5-0, kwenye Azam Complex. Muda alipokea pasi ya aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Hafiz Konkoni akamchungulia kiufundi kipa Wilbol Maseke kwa mbali kisha kufunguka kwa ufundi wa hali ya juu.


Yanga vs Namungo 1-0

Kiungo huyo aliifungia Yanga bao pekee kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo, akitokea benchi dakika ya 67 na wakati wengi wakidhani mechi hiyo itaisha kwa sare alibadilika na kucheza kama namba 10 na alipokea pasi safi ya beki Yao Attohoula, ndani ya eneo la sita kisha akamalizia kwa ustadi mzuri.


Yanga vs Dodoma Jiji 1-0
Hakuishia hapo, Gamondi alinogewa na kumpa tena nafasi Mudathir akicheza kama kiungo mshambuliaji tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Alifanya kweli dhidi ya Dodoma na  akipokea pasi ya beki wake wa kushoto Nickson Kibabage nje kidogo ya sita, alifunga bao la ushindi dakika ya 85 kwenye mchezo uliokuwa na presha kubwa ikionekana kama wenyeji wataambulia sare, kabla ya kiungo huyo kuiokoa dakika za mwisho akicheza kiungo wa juu.


Yanga vs Mashujaa 2-1
Mudathir aliyetua Yanga akiwa kama mchezaji huru msimu uliopita aliendeleza moto akicheza kama kiungo wa juu na dakika ya 85, tena anaitumia kufunga bao muhimu la ushindi ndani ya eneo la sita akimalizia pasi ya mshambuliaji Kennedy Musonda na kuiongoza timu yake kushinda 2-1.


KMC vs Yanga 3-0
Moto wa mabao ya Mudathir uliendelea tena mbele ya KMC akiwafunga makipa wawili tofauti wa timu hiyo kwenye mchezo mmoja akitangulia kumfunga Maseke dakika ya kwanza tu akitumia makosa ya kipa wa wenyeji mpira aliokuwa anauhamisha kipa huyo ukamkuta mshambuliaji Clement Mzinze kisha kiungo huyo kuachia shuti kali na beki kuokoa.


Akaendelea kubaki mchezoni na kujikuta ananufaika na mpira uliotemwa na Maseke kutokana na shuti la Stephanie Aziz Ki na kuunasa na kuukwamisha wavuni.


Bao lake la sita alilifunga dakika ya 53, safari hii akimfunga kipa wa pili, Denis Richard kwenye shambulizi ambalo alilianzisha mwenyewe katikati ya uwanja kisha akabaki mchezoni na kwenda kupokea pasi safi ya Kibabage akiwa ndani ya eneo la hatari na kuipa timu yake  bao la pili.


Kiungo huyo alisema kupata namba ndani ya kikosi cha Yanga inategemea na namna ulivyomshawishi kocha kwenye mazoezi.
“Gamondi ananipa majukumu yote uwanjani, kukaba, kuchezesha timu na kushambulia kwa kufika ndani ya boksi, nitafunga sana, nimeambiwa nifanye yote kwa sababu ya uwezo wangu wa kucheza nafasi nyingi uwanjani.


“Sijaanza kucheza soka jana au juzi nina misimu mingi lakini msimu huu nimekuwa nikifunga kwa sababu nimekuwa nikijitoa na kujituma kwa kuhakikisha nafanyia kazi mipango ya kocha,” alisema.


Alisema Gamondi amekuwa akimsisitiza kujiongeza akiwa uwanjani, pia kutokana na ubora wa wapinzani wake unampa nguvu na kujiamini.


SIMU BAADA YA BAO
Kiungo huyo amefunguka staili yake ya ushangiliaji ni maalumu kwa familia yake mke na mwanaye kwa sababu ni watu ambao amekuwa akiwasiliana nao mara kwa mara.


“Nimekuwa nikishangilia hivyo kama salamu kwa familia yangu ambayo sina muda mwingi wa kukaa nao karibu hasa nikiwa kambini, hivyo nimekuwa nikitumia simu kuzungumza nao mara kwa mara;


“Sina maana nyingine yoyote japo kila mtu amekuwa akitafsiri anavyojisikia yeye lakini kwa upande wangu ndio hivyo nilivyokwambia ni simu kwa mke na mtoto,” alisema Mudathir.


CHAMAZI HASHIKIKI
Kiungo huyo amefunga mabao manne kati ya sita aliyonayo msimu huu akiutumia Uwanja wa Azam Complex ambao amekuwa na nyota nao huku mabao mawili pekee akiyafunga nje ya Dar es Salaam, akiwafunga KMC, Jamhuri, Morogoro.

KMC chaka lake
KMC ndio timu aliyoifunga zaidi Mudathir akiwafunga mabao matatu ndani ya msimu mmoja hadi sasa, huku Dodoma akiwafunga mabao mawili lakini kila bao akiwafunga msimu mmoja.

DAKIKA
Kiungo huyo amecheza dakika 972, kwenye mechi 14 kati ya 16 zilizochezwa na timu hiyo huku akihusika kwenye mabao saba kati ya 39 yaliyofungwa na Yanga.


Amefunga mabao sita dhidi ya KMC, Namungo, Dodoma Jiji, Mashujaa na mawili dhidi ya KMC huku akitoa asisti kwenye mechi dhidi ya Geita Gold.