Mtaalamu Simba amrahishia kazi Gomes

Tuesday February 23 2021
mtaalam pic
By Thobias Sebastian

ZIMEBAKI saa chache kabla ya Simba kushuka uwanjani kuvaana na Al Ahly katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mtaalamu aliyeletwa kutoka Zimbabwe, Culvin Mavunga akimrahisishia kazi Kocha Didier Gomes ili kuwamaliza Waarabu jijini Dar es Salaam.

Wekundu wa Msimbazi, wamekuwa na mzuka mwingi kwenye mchezo huo ambao kiingilio chake cha chini kikiwa ni buku tatu (Sh3,000) kwani wamekuwa wakijifua wakitumia utaalamu wa Mavunga aliyeletwa na mabosi wa Simba akitokea nchini Zimbabwe.

Usichokijua ni Simba msimu huu moja ya silaha wanazotumia kufanya vizuri ni mtaalamu wao wa masuala ya uchambuzi wa mechi kupitia runinga, yaani Mavunga ambaye tangu atue benchi la ufundi na wachezaji wamekuwa wakilainisha mambo kisasa.

Mwanaspoti lililofichua ujio wa mtaalamu huyo aliyeanza kazi yake ya kwanza katika mechi ya ugenini dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe alieleza baadhi ya mambo aliyoyaona katika mechi hiyo ya leo.

Mavunga alisema katika kikosi chao wanaendelea kufanya maandalizi ya kutosha ili kuboresha mapungufu waliyokuwa nayo na kuimarika katika maeneo ambayo wamekuwa na ubora tangu kuanza kwa mashindano hayo.

“Shida yetu Simba ya kwanza kubwa tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga ambazo kati ya hizo tunatumia chache kwenye mechi za timu aina ya Al Ahly ukifanya hivyo maana yake utakuwa umepoteza mechi,” alisema Mavunga ambaye unaweza kumchukulia poa jinsi alivyo aliyeongeza;

Advertisement

“Ebu angalia mechi iliyopita tumepata nafasi tatu za wazi na kufunga mabao tumetumia moja kwenye mchezo na Al Ahly sioni nafasi ya kuzipata kama hizo maana yake hata moja tu inatakiwa kutumiwa vizuri.”

“Tumewaangalia wapinzani wetu, wana ubora katika maeneo mengi ndio maana timu ya tatu duniani ila kuna mapungufu ambayo tumeyaona kutoka kwao na tumeanza kuyafanyia kazi na kocha mkuu pamoja na wachezaji,” alisema Mavunga.

Mtaalamu huyo alisema kutokana na hali ilivyo si rahisi kueleza mambo yao mengi kwani itakuwa ni kama kuuza silaha wakati wa vita, ila alisisitiza kuwa Simba imejipanga kufanya vizuri kama katika mechi zilizopita na kusisitiza kilichobaki kwa sasa ni bosi na vijana wake kwenda kumalizia kazi.

“Tunaendelea na mazoezi wakati huu ili kuwapatia wachezaji kile ambacho kinastahili kulingana na ubora, mapungufu waliyokuwa nayo wapinzani wetu ili kuwazidi na kama tafanya vile ambavyo tunawaelekeza ushindi unawezekana,” alisema Mavunga.

Kocha Gomes, alisema wameshaisoma Al Ahly na kujua uimara na udhaifu wao na wanaenda kufanya kile ambacho mashabiki wao wana hamu ya kukiona kwa kupata matokeo mazuri kama ilivyokuwa kwenye mechi yao ya ugenini dhidi ya AS Vita ya DR Congo waliposhinda bao 1-0.

Simba na Al Ahly wanakutana jijini Dar es Salaam ikiwa imetimia miaka miwili kamili tangu Meddie Kagere alipofunga bao pekee wakati Mafarao hao wakilala kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika ligi ya msimu wa 2018-2019 na Simba kulipa kisasi cha kipigo cha mabao 5-0 jijini Cairo.

Advertisement