Msuva kuongoza vita ya Amakhosi

Muktasari:
BAADA ya kuiangamiza klabu yake ya zamani Difaa El Jadida, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva anayecheza soka la kulipwa Morocco, anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya chama lake la Wydad Casablanca, keshokutwa Jumatano kwenye mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chief ya Afrika Kusini.
BAADA ya kuiangamiza klabu yake ya zamani Difaa El Jadida, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva anayecheza soka la kulipwa Morocco, anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya chama lake la Wydad Casablanca, keshokutwa Jumatano kwenye mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chief ya Afrika Kusini.
Amakhosi ndio walioing’oa Simba kwenye hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao 4-3 na sasa watavaana na Wydad ambayo jana ilikuwa ugenini katika Ligi Kuu ya Morocco kuumana na Hassania Agadir ikiwa ni siku chache tangu walipoibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Difaa ambayo aliwahi kuichezea Msuva, aliyewapiga bao moja kali la video kwenye kipigo hicho.
Bao hilo la kideo, Msuva alilifunga akiwa ndani ya penalti boksi, akimalizia krosi kutoka wingi ya kushoto, mpira ule ulidunda naye akajipinda na kuupiga kwa namna yake, uligonga nguzo ya juu na kuzama kisha kutoka nje, alikuwepo mchezaji mwingine wa Wydad alimalizia lakini ilionekana mpira ule ulishazama awamu ya kwanza.
Kwa mujibu wa kocha wa Wydad, Mtunisia Faouzi Benzarti alitumia michezo hiyo miwili ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuwavaa wababe wa Simba, Amakhosi licha ya kwamba walikutana nao kwenye hatua ya makundi.
Akiuzungumzia mchezo huo wa nusu fainali, Msuva anaamini utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu hizo mbili kukutana mara mbili kwenye michezo ya hatua ya makundi.
“Kuna-weza kuonekana mabadiliko makubwa, unajua mbinu za michezo ya hatua ya makundi huwa tofauti na mtoano kwa hiyo mchezo unaweza kuwa mgumu sana,” akisema Msuva na kuongeza;
“Tutaanzia nyumbani, nadhani tuna jukumu moja tu muhimu la kutafuta msingi mzuri ambao utatufanya tusiwe watumwa tukiwa ugenini. Kwa upande wa maandalizi kwetu yameenda vizuri.”
Wydad na Kaizer zilishakutana kwa mara ya kwanza Februari 28 mwaka huu katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mchezo huo ulimalizika kwa chama la Msuva kuibuka na ushindi mnono wa 4-0 na katika marudiano wakapelekea kikosi B na Wamorocco hao walicharazwa 1-0.
Wydad ilipelekea kikosi hicho kwa vile ilikuwa tayari imejikatia tiketi ya kucheza robo fainali hivyo waliamua kupumzisha majembe yao akiwamo Msuva, huku wakitoa nafasi zaidi kwa kikosi chao cha vijana ili wapate uzoefu kwenye mashindano hayo makubwa.