Prime
Mrithi wa Dube asakwa Ulaya

Muktasari:
- Ni kama ndoa ya Azam na Dube ipo ukingoni kuvunjika jambo ambalo limewafanya matajiri hao wa Chamazi kuanza mapema mchakato wa kutafuta mshambuliaji mwingine ambaye anaweza kuongeza nguvu katika kikosi cha Youssouph Dabo kwa ajili ya msimu ujao wa 2024/25.
WAKATI Prince Dube akiendelea kuipasua kichwa Azam FC kwa kuipeleka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akitaka aachiwe aendelee na maisha yake, tayari mabosi wa timu hiyo wameripotiwa kuwa na majina matatu mezani ya washambuliaji akiwamo mmoja wa Kiganda kutoka Ulaya kwa ajili ya kuziba pengo la Mzimbabwe huyo.
Ni kama ndoa ya Azam na Dube ipo ukingoni kuvunjika jambo ambalo limewafanya matajiri hao wa Chamazi kuanza mapema mchakato wa kutafuta mshambuliaji mwingine ambaye anaweza kuongeza nguvu katika kikosi cha Youssouph Dabo kwa ajili ya msimu ujao wa 2024/25.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, inaelezwa miongoni mwa washambuliaji hao ni pamoja na Sadat Anaku, ambaye anacheza soka la kulipwa Scotland akiwa na Dundee United ambayo inashiriki ligi daraja la kwanza nchini humo (Scottish Championship).
Akiongelea uwepo wa majina hayo, Dabo alisema, "Nina faida ya kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja, kwa sasa tutaendelea na mapambano ili kumaliza vizuri msimu, tunaamini tunaweza kufanya kitu, baada ya hapo ndio tunaweza kuongea kuhusu maboresho ya kikosi."
Sadat, ambaye aliwahi kufanya vizuri katika ligi ya Uganda akiwa na KCCA, amekuwa katika wakati mgumu huko Scotland kutokana na kusumbuliwa na majeraha, amefunga bao moja tu katika michezo 14 tangu ajiunge na timu hiyo huku akicheza kwa dakika 338 kati ya 1260.
Mkataba wa mshambuliaji huyo na Dundee unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, mpaka sasa hakuna mazungumzo yoyote ambayo yameripotiwa juu ya kuongezewa mkataba mpya hivyo hiyo ni habari njema kwa Azam FC.
Kwa sasa Azam imesaliwa na mshambuliaji mmoja tu wa kati ambaye ni Franklin Navarro kutokana na Alassane Diao kusumbuliwa na majeraha ambayo huenda yakamweka nje ya uwanja hadi mwishoni mwa msimu.