Morrison ashtukiwa, apewa wiki mbili Yanga

Morrison ashtukiwa, apewa wiki mbili Yanga

BERNARD Morrison ameanza kazi rasmi Yanga na leo akiingia siku ya nne mazoezini, lakini kocha mmoja fundi wa mazoezi ameshtukia kitu kwa winga huyo Mghana kisha akamtengea siku 14 za kazi nzito.

Kocha aliyemshtukia BM33 ni Helmy Gueldich ambaye ni kocha wa mazoezi ya viungo aliyeangalia ubora wa mshambuliaji huyo kisha akagundua kwamba jamaa hakufuata sawasawa ratiba ya mazoezi waliyomtumia.

Helmy hata hivyo ameliambia Mwanaspoti kwamba Morrison yuko nusu fiti - nusu unga, lakini ndani ya wiki mbili tu atakuwa katika daraja lingine la ubora.

Kocha huyo alisema katika ratiba ya wiki ya kwanza Morrison atakuwa na kazi ngumu ambayo itamsaidia baadaye kurudisha ubora.

“Tulimpatia ratiba mapema kabla ya kujiunga alitakiwa kuifanya kwa ukamilifu lakini nimemuangalia naona hakuifuata sawasawa ila atakuwa sawa,” alisema Helmy ambaye bado anahitajika Chama cha Soka Tunisia.

“Ni mchezaji mzuri (Morrison) sio mbaya kwa hali aliyokuja nayo kitu kibaya angekuwa hajafuata kabisa lakini tuna muda wa kumrudisha katika mstari.”

Juzi Morrison alikimbizwa mazoezini Yanga akizunguka peke yake pembeni kisha akasimama na kulalamika akiongea kwa Kiswahili akisema: “Huyu jamaa anaiua huyu’ kauli ambayo mashabiki waliokuwa wakiangalia mazoezi hayo nje ya uzio walijikuta wakicheka huku wakishangilia.

Helmy ndiye aliyempunguza uzito beki Djuma Shaban kwa kilo tano kutoka 85 na kubaki na 79 hatua ambayo kocha Nasreddine Nabi amechekekelea akidai beki huyo atakuwa bora zaidi msimu ujao.

Wakati Helmy akimfua Morrison, kocha Nabi amefichua anajipanga kufanya kikao maalumu na winga huyo mwenye mbinu za kupangua ukuta.

Nabi alisema anaamini Morrison atakuwa ni mwiba mkali kwa wapinzani msimu ujao, lakini anataka kukaa naye wakiwa wawili tu kumpa mwelekeo wa maisha ndani ya kikosi hicho.

“Sifanyi hivi kwa Morrison peke yake nimeshazungumza na wengine wote ambao wamekuwa wakifika hapa. Ni vizuri akajua maisha yetu hapa na kitu gani tunakitaka kwake na vitu gani hatakiwi kuvifanya hapa,” alisema.

“Kila mmoja anampenda mchezaji mcheshi na hasa Morrison. Huyu ni mchezaji ambaye tumemsajili kwa mahitaji ya timu hasa malengo yetu kwa msimu unaokuja.”

AGEUKA GUMZO

Kama ulikuwa unadhani BM33 kabadilika kwa vituko pole yako, kwani jamaa amegeuka gumzo kwa wachezaji wenzake wakati wa utambulisho na kusababisha Nabi kupigwa butwaa.

Ipo hivi. Wakati wa utambulisho wa wachezaji wapya ilipofika zamu ya Morrison, kocha Nabi alimtaka ajitambulishe ndipo akafanya timu nzima iangue kicheko.

Morrison akiwa uso mkavu alimjibu Nabi; “Jamani... jamani kocha ujitambulishe wewe, mimi ni mwenyeji hapa.” Jambo ambalo lilimfanya Nabi ashindwe uvumilivu na kuangua kicheko.

Wakati kocha Nabi anaendelea kucheka, Morrison aliendelea na utani wake kwa kuwauliza wachezaji aliocheza nao kabla ya kuhamia Simba alikocheza 2020-2022.

“Nyie mliokuwepo eti hamnifahamu jamani...jamani, wewe Fei Toto na wewe hunifahamu.” Jambo lililofanya timu nzima wacheke wakishindwa kuvumilia kuendelea kumsikiliza.

Hata hivyo, ilimlazimu kocha amwambie apunguze utani na ajitambulishe kisha waendelee na mazoezi na akafanya hivyo.

Wachezaji wa timu hiyo ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema hadi sasa mchezaji anayeongoza kwa ucheshi na vituko huko kambini ni Morrison anayejichanganya na kila anayemuona mbele yake.

Nje na wachezaji waliyopo Yanga sasa hivi, ambao walicheza naye na wapo na timu nyingine waliyasimulia maisha yake awapo kambini.

Beki wa zamani wa timu hiyo, Juma Makapu ambaye kwa sasa kasajiliwa Ihefu FC alisema Morrison ana vituko na anapokuwepo hapawezi kukosekana mizaha.

“Ni asili yake siyo mambo anayojifunza mnaweza mkaaa na kila mtu akawa na mambo yake anatoka anakotoka anaanza mizaha, naamini huko Avic Town watakuwa na kicheko,” alisema.

Kauli yake iliungwa mkono na Adeyum Saleh ambaye kwa sasa anakipiga Geita Gold “Jamaa ni mcheshi anaweza akaibua jambo hadi ukashangaa, naamini waliyopo kambini watakuwa wanacheka sana.”