Morrison aja na dawa ya Yanga

Muktasari:

STAA mwenye vituko wa Simba, Bernard Morrison jana alirejea nchini kimyakimya, kisha akatoa tamko kuelekea mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Yanga utakaochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

STAA mwenye vituko wa Simba, Bernard Morrison jana alirejea nchini kimyakimya, kisha akatoa tamko kuelekea mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Yanga utakaochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Morrison alienda kwao Ghana huku akiacha taharuki kuwa mshambuliaji huyo ameondoka akiwa na shida na uongozi wa klabu madai ambayo mabosi wa wa timu hiyo waliyakanusha.

Jana, Morison aliwasili nchini na Mwanaspoti lilimnasa akitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akipokewa na jamaa zake wawili.

Akizungumza mara baada ya kuwasili, Morrison alisema: “Nimerudi kazini, nimemaliza mapumziko, sasa narudi kufanya kazi yangu katika klabu yangu.”

Morrison ambaye ni maarufu kwa jina la Mzee wa Kuwakera aliongeza kuwa: “Nipo tayari kwa mchezo huo (dhidi ya Yanga), ndio maana nasema nimerudi kazini, safari hii sitaki kuongea sana nataka kufanya vitu kwa vitendo zaidi.”

Tangu atue Simba, Morrison amekutana na Yanga mara tatu na mechi ya kwanza alishindwa kucheza akiwa jukwaani kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi akiishuhudia timu yake ikitolewa kwa matuta huku wapinzani wake wakichukua kombe hilo.

Mchezo wa pili wa ligi, Morrison alikosekana kufuatia kusimamishwa na mechi ya tatu licha ya kucheza aliishuhudia Simba ikilala bao 1-0 na sasa Julai 25 atakutana na Yanga kwa mara ya nne akiwa na jezi ya Simba.