Mmesikia Chama hukoo

BAO la ushindi dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe juzi, limeendeleza historia tamu ya kiungo Clatous Chama ya kufunga mabao yanayoihakikishia ushindi Simba na kuivusha kutoka hatua moja kwenda nyingine.

Katika mchezo huo ambao Simba waliibuka na ushindi wa mabao 4-0, Chama alifunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penati na kuifanya Simba ifuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1.
Hata hivyo hiyo ni mara ya nne kwa Chama kufanya hivyo kwani hapo kabla alishawahi kufanya kitu kama hicho katika mechi kadhaa za kimataifa.

Nyota ya bahati kwa Chama ilianza kumuwakia Novemba 28, 2018 pale alipoifungia Simba bao la mwisho dhidi ya Mbabane Swallows ya Eswatini katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya amshindano hayo uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini ambao waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 ingawa katika mechi ya marudiano waliyoshinda kwa mabao 4-0, ugenini, bao la mwisho lilipachikwa na Meddie Kagere japo Chama alifunga mabao mawili katika mechi hiyo.
Chama aliendeleza balaa lake kwa kufunga bao la tatu katika mechi dhidi ya Nkana iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao ulikuwa wa marudiano wa hatua ya kwanza na kuifanya Simba iibuke na ushindi wa mabao 3-1 uliowapeleka hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu huo.
Chama tena alikuja kufunga bao la mwisho ambalo pia liliivusha Simba na kuipeleka katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo msimu huohuo katika mchezo wa mwisho dhidi ya AS Vita ya DR Congo ambao ulichezwa katika uwanja huohuo ambapo Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Maajabu ya Chama yakajirudia tena msimu huu ambapo alifunga bao pekee la ugenini dhidi ya Plateau ya Nigeria lililoivusha Simba kutinga raundi ya kwanza kwa ushindi wa bao 1-0.
Chama kwa mara nyingine tena akafunga hesabu kwenye mechi ya juzi bao la nne kwa mkwaju wa penati ambayo ilipatikana baada ya kufanyiwa faulo ndani ya eneo la hatari.
Kiungo huyo mshambuliaji amekuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Simba kutokana na mchango wake hasa katika kupika mabao lakini pia hata kufunga tangu alipojiunga 2018.
Katika msimu uliopita, Chama alipiga pasi za mwisho 12 na kufunga mabao matano kwenye Ligi Kuu jambo lililomwezesha achaguliwe kuwa mchezaji bora wa msimu.