Miquissone: Nilimfunga Al Ahly kuwaonyesha

WINGA wa Simba, Luis Jose Miquissone amesema bao alilofunga dhidi ya Al Ahly limezidi kumtengenezea heshima mbele ya kocha, Pitso Mosimane ambaye alianza kufanya naye kazi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Alimfunga makusudi ili kumuonyesha kitu. “Hata aliposema ni moja ya wachezaji hatari katika kikosi cha Simba wala hakukosea kwa vile ananifahamu vizuri na anaelewa mambo mengi kutoka kwangu jambo ambalo lilisababisha niweze kujiandaa na kujituma zaidi,” alisema.

“Nilitenga muda zaidi wa kujiandaa kwa kutambua nilikuwa nakwenda kucheza mechi kubwa lakini dhidi ya timu ambayo kocha wake nafahamiana naye na natakiwa kumuonyesha kuwa nimeimarika zaidi ya mara ya mwisho tulivyoonana.

“Kile ambacho nilipanga kwenda kukionyesha uwanjani nashukuru kwa kiasi kikubwa nimekifanikisha na kuifungia timu yangu bao muhimu ambalo tulikuwa tunalihitaji na limeamua mechi,” alisema Miquissone.

“Kweli bao ni zuri kutokana na aina yake ya ufungaji lakini uzuri zaidi ulianzia tangu mwanzo wa kutengeneza shambulizi ambalo lilitokana na mchango wa wachezaji wenzangu ambao wamefanya kazi nzuri na niwapongeze kwa hilo,” alisema.

Alisema ushindi huo kama timu walikuwa wanauhitaji zaidi ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye kundi na kufikia malengo ya kucheza nusu fainali ya mshindano hayo makubwa.

“Kufunga bao dhidi ya Al Ahly si jambo dogo kama mchezaji limenipa ari na morali ya kuendelea kujituma zaidi kwani nina imani kutakuwa na mafanikio ndani yake kwa timu na binafsi.

“Tuendelee kushirikiana kwa kila mmoja kutimiza majukumu yake na kwa nafasi yake. Nina imani Simba hii itafika mbali katika mashindano haya ya kimataifa pengine zaidi ya inavyodhaniwa na hilo linatokana na ubora wa wachezaji waliopo ndani ya kikosi,” alisema.