Minziro ashusha pumzi, JKT Tanzania kiroho safi

Muktasari:
- Pamba Jiji imebaki Ligi Kuu baada ya juzi kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kufikisha pointi 33, ikipanda hadi nafasi ya tisa katika msimamo na kujiweka pazuri kutokana na matokeo ya timu nyingine katika mstari wa mechi za play-offs.
WAKATI maafande wa JKT Tanzania wakisema hawana wa kumlaumu kwa kipigo walichopewa na Pamba Jiji kwani kwani malengo kwa msimu huu yapo sawa, kocha Fred Felix ‘Minziro’ ameshusha pumzi ndefu baada ya kuisaidia timu hiyo kubaki Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao, huku akitoa ushauri.
Pamba Jiji imebaki Ligi Kuu baada ya juzi kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kufikisha pointi 33, ikipanda hadi nafasi ya tisa katika msimamo na kujiweka pazuri kutokana na matokeo ya timu nyingine katika mstari wa mechi za play-offs.
Kabla ya mechi juzi, Pamba ilikuwa inakamata nafasi ya 12 ikiwa na pointi 30, lakini ushindi huo umemfanya Minziro, kusema anashukuru kujinusuru kwani haikuwa kazi rahisi mbele ya maafande hao ambao nao hawakuwa salama.
“Vijana walisema mbele ya Mkuu wa Mkoa na Mkurugenzi mechi ya leo (juzi) ni kufa au kupona lazima tupate matokeo, nadhani Pamba sasa haiko kwenye hatari au kucheza playoffs (mtoano),” alisema Minziro na kuongeza;
“Niliwaambia vijana wangu tunaposhinda mechi ya JKT Tanzania tunakuwa tumemaliza kila kitu Pamba inakuwa iko salama kwa msimu ujao. Najisikia faraja kubwa kwa kujua unakutana na timu ambayo haikuwa katika hali nzuri na haikuwa na usajili mzuri ulio bora lakini dirisha dogo walau tukaongeza nguvu, kusema ukweli vijana wamejitahidi.”
Minziro aliongeza kwa kusema; “Nawashauri pengine msimu ujao makosa ambayo yamefanyika msimu huu pengine hayatojirudia.”
Kwa upande wa kocha wa JKT TZ, Ahmad Ally amesema bado hajafikia kiwango anachotamani kuwapo katika safari yake ya ualimu, lakini anashukuru kumaliza salama msimu huu.
Ally ni kocha pekee mzawa katika Ligi Kuu Bara msimu huu ambaye hajafukuzwa na kufanikiwa kumaliza msimu akiwa na kikosi hicho, huku akiwa ni kocha wa pili ambaye hakufungashiwa virago katika ligi akiungana na kocha wa Simba, Fadlu Davids.
Kocha huyo ameitengeneza JKT Tanzania kuwa tishio, ambapo inakamata nafasi ya saba baada ya michezo 29.
Imevuna alama 35, ikishinda mechi nane, sare 11 na kupoteza tisa huku ikiwa imefunga mabao 27 na kuruhusu 27.
Alisema anafarijika kuona wadau wanapendezwa na anachokifanya ndani ya kikosi hicho kwani kila nyakati anayoipitia inamsaidia kujifunza na kujijenga kwenye wakati mzuri na mbaya.
“Kwenye kazi yangu nahitaji kuwa bora zaidi ya hapa nilipo kwani bado naona sijafikia kile ambacho natamani kukifikia, namuomba Mungu aniongoze nisibweteke kwenye hizi sifa ninazopewa,” alisema Ally.
Alisema licha ya kubakiza mchezo mmoja wa ligi lakini kwa hatua waliyopo malengo ya klabu kusalia kwenye ligi na kuwa na timu bora ambayo inaweza kupambana kwenye aina ya mechi zote, yametimia.
“Nafikiri ndani ya hayo malengo hatujatoka kwani msimu ulioisha JKT Tanzania ilikuwa kwenye playoffs (mechi za mtoano kuwania kutoshuka daraja). Kwa sasa tunapambana tu kumaliza katika nafasi nzuri, ila tuangalie msimu ujao nini tunaweza kuboresha zaidi kwa wachezaji hawa wazawa,” alisema.