Mfaransa rasmi Yanga

KAZI imeisha. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mabosi wa Jangwani kuamua kwa pamoja kulipitisha jina la Mfaransa Hubert Velud kuwa Kocha Mkuu wao kuchukua mikoba ya Cedric Kaze, lakini wakimpa rungu Kocha Juma Mwambusi kuiongoza timu hadi mwisho wa msimu huu.
Mabosi hao wa Yanga walikuwa wanakuna kichwa kulipitisha jina moja kati ya matatu waliyokuwa nayo mkononi na mwishowe wakakubaliana kocha huyo wa zamani wa TP Mazembe anayeifundisha kwa sasa timu ya taifa ya Sudan ndiye anayewafaa.
Majina mengine yaliyokuwa katika tatu bora kama Velud angezingua, ni pamoja na kocha wa zamani wa Simba anayeinoa kwa sasa AFC Leopards ya Kenya na Benito Floro ambaye ni mgeni katika soka la Afrika, lakini naye aliwaridhisha vigogo wa Yanga kwa wasifu wake wa kusisimua.
Chanzo makini cha habari kutoka ndani ya Yanga na kingine kilichopo Sudan kinasema kuwa, mabosi hao wamekubaliana na Kocha Velud kuinoa timu yao, lakini mwenyewe akitaka aje Julai mara baada ya kumalizika kwa msimu huu, ili kupanga jeshi lake mwenyewe ikiwamo kuchagua wachezaji anaowataka ili kusiwe na kisingizio mbele.
Kutokana na msimamo wa Mfaransa huyo mabosi hao wamekubaliana katika mechi 11 za Ligi Kuu Bara zilizosalia kwa timu yao, zisimamiwe na Kaimu Kocha Mkuu wa sasa Juma Mwambusi ambaye alipewa nafasi ya kuchagua wasaidizi wake watatu wa kufanya nao kazi akiwamo kocha wa makipa, baada ya dili la Mfaume Athuman kutoka Dodoma Jiji kukwama kwa sababu ya mkataba wake.
“Yanga imekubaliana na Velud kuja kuinoa, lakini hatakuja sasa, badala yake ni mpaka msimu uishe, ila atakuja mapema ili alitengeneze jeshi lake mwenyewe na kwa muda uliobaki, Mwambusi ndiye atakayesimamia timu na amepewa nafasi ya kuchagua makocha watatu anaotaka kufanya nao kazi,” chanzo makini kutoka ndani ya Yanga kiliithibitishia Mwanaspoti.
Mfaume Athuman, kipa wa zamani wa Yanga alikuwa kwenye nafasi kubwa ya kujiunga na Yanga kuchukua nafasi ya Vladimir Niyonkuru aliyefurushwa sambamba na Kaze na Nizar Khalfan baada ya vinara hao wa Ligi Kuu kulazimishwa sare ya 1-1 na Polisi Tanzania wiki iliyopita, lakini mkataba wake na klabu yake ya sasa na Dodoma Jiji umewafanya mabosi wa Jangwani kumpotezea.
“Mwambusi ana uamuzi wa kusema aletewe makocha gani watatu wa kufanya nao kazi akiwamo kocha msaidizi na wa makipa, ili kuhakikisha mechi zilizosalia za ligi zinamalizika vyema sambamba na kuhakikisha anafanya vizuri kwenye Kombe la ASFC,” chanzo hicho kiliongeza.
KIDOGO KITIBUKE
Kabla ya dili hilo la Velud kutiki, Mfaransa huyo aliwapa ugumu mabosi wa Yanga kwa kutoa sharti ambalo nusura litibue, lakini vigogo wa Jangwani walikaa chini na kujadiliana na kuamua freshi.
Taarifa kutoka Sudan ni kwamba Velud aliwaambia Yanga wafike mshahara wa dola 20,000 na kuwafanya mabosi hao kukuna kichwa, kwani dau lao lilikuwa chini ya hapo na baadhi yao waliona kiasi hicho cha fedha ni kikubwa, lakini wasifu wake unawafanya wabadilishe mawazo.
Inaelezwa mipango ilikuwa kama wangeshindwana na dau hilo la Velud, Yanga ilikuwa ipiga hesabu ya kumrudisha nchini kocha wa zamani wa Simba, Patrick Aussems ‘Uchebe’ anayeinoa kwa sasa AFC Leopards ya Kenya, kwani dau lake halikuwa kubwa kulinganisha la Mfaransa huyo.
Chaguo la tatu lilikuwa ni Mhispania Benito Floro ambaye licha ya jina lake kubwa shaka inakuja kwamba kama ataweza kumudu soka la Afrika sambamba na maslahi yake pia.
Ndipo ikaamuliwa ni vyema kuwa na Velud ili aje kuwapa mataji, hasa kwa vile Yanga ina msimu wa tatu mfululizo ikiwa haina taji lolote la Ligi Kuu Bara wala lile la Kombe la ASFC inayotoa nafasi ya uwakilishi wa michuano ya kimataifa kwa timu yao.
VELUD NI NANI?
Hubert Velud, alizaliwa Juni 8, 1959 katika mji wa Villefranche-sur-Saone, nchini Ufarasna na alianza kucheza soka miaka ya 1970 katika klabu ya Reims. Klabu hii aliichezea kati ya 1976-1989 alipohamia Chalons-sur-Marne iliyokuja kuifundisha pia. Klabu nyingine alizozifundisha ni Paris FC, gazelec Ajaccio, Clermont, Creteil, Toulon, Beauvais kabla ya kuifundisha timu ya taifa ya Togo kati ya 2009-2010.
Kocha huyo anayesifika kwa soka la kitabuni na lenye kushambulia zaidi, ni mzoefu katika soka la Afrika kwani amezifundisha klabu kadhaa na kutwaa nao mataji kabla ya kutua Sudan anakkoinoa kwa sasa timu ya taifa hilo.
Klabu kubwa alizofundisha Afrika na zinazomfanya kuwa mmoja wa makocha wenye uzoefu mkubwa kwa soka la bara hili ni pamoja na Hassania Agadir ya Morocco, ES Setif, US Alger na CS Constantine za Algeria, TP Mazembe ya DR Congo, Difaa El Jajida ya Morocco, aliyowahi kuichezea Saimon Msuva kisha kuhamia JS Kabylie ya Algeria hadi mwaka jana kabla ya kutua Sudan.
Velud ametwaa mataji kadhaa akiwa na timu alizofundisha ikiwamo Clermont ya Ufaransa aliotwaa ubingwa wa Taifa 2001-2002 kisha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Algeria akiwa na ES Setif mwaka 2013, akabeba Super Cup nchini Algeria akiwa na USM Alger 2013 na ubingwa wa Ligi Kuu 2014 kabla ya kuhamishia makali DR Congo akiwa na Mazembe, likiwamo taji la CAF Super Cup 2016.