Mfaransa ana balaa!

Muktasari:
Japo Kocha wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre aliwaka kwa mastaa wake hao kupewa kadi, lakini halijawahi kuwa tatizo kabisa kwake katika kuziba nafasi hizo.
JUMANNE Simba itashuka dimbani kuikabili Mtibwa Sugar pale Jamhuri mjini Morogoro, lakini bila mastaa wake Erasto Nyoni, Juuko Murhid na James Kotei ambao wote wanakadi tatu za njano.
Japo Kocha wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre aliwaka kwa mastaa wake hao kupewa kadi, lakini halijawahi kuwa tatizo kabisa kwake katika kuziba nafasi hizo.
Sasa angalia alichokifanya huyu fundi wa Kifaransa, kwenye mazoezi ya kikosi chake amekuwa akiwajaribu wachezaji kadhaa kama watafiti kuziba nafasi hizo.Miongoni mwa wachezaji wanaojaribiwa yumo fundi wa Kinyarwanda, Haruna Niyonzima ambaye amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.
“Inanilazimu kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao hawajacheza muda mrefu,” alisema.
Mbali na Niyonzima, wengine ambao wanapewa nafasi kubwa ya kuziba nafasi hizo dhidi ya Mtibwa Sugar ni beki wa kati Asante Kwasi, ambaye anaweza kutumika kama beki wa kushoto na nafasi yake kuzibwa na Mohammed Hussen ‘Tshabalala’, ambaye hana namba ya uhakika kwenye kikosi cha kwanza.
Eneo la kiungo mkabaji, ambapo Kotei atakosekana Jonas Mkude atachukua nafasi hiyo, ambapo kwa sasa majeruhi yake yanaendelea vizuri. Nafasi ya kiungo mshambuliaji ambayo Nyoni atakosekana, ataingia Said Ndemla, Niyonzima ama Mzamiru Yassin.