Mdhamini aitoa hofu Tanzania Prisons

Muktasari:

  • Oktoba 29 mwaka jana, Prisons ilisaini mkataba wa udhamini wa kampuni hiyo kwa thamani ya Sh 150 milioni, ambapo Mwalunenge akiahidi bonasi na ofa mbalimbali.

MKURUGENZI wa kampuni ya Bens Agro Star, Patrick Mwalunenge amewatoa hofu Tanzania Prisons kuwa ahadi alizotoa kwenye mkataba wa kuidhamini timu hiyo atazitekeleza na kuongeza mkataba mpya msimu ujao.

Oktoba 29 mwaka jana, Prisons ilisaini mkataba wa udhamini wa kampuni hiyo kwa thamani ya Sh 150 milioni, ambapo Mwalunenge akiahidi bonasi na ofa mbalimbali.

Bonasi hizo ni mchezaji bora wa msimu kwa timu hiyo kujengewa nyumba ya kisasa, Sh 10 milioni kwa ushindi wa Simba na Yanga, Sh 1 milioni kwa bao na Sh 500,000 kwa Kocha Mkuu kila ushindi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwalunenge alisema baada ya ligi kuisha anatarajia kukaa meza moja na wachezaji na viongozi wa timu hiyo kufanya tathimini na lengo kubwa ni kulipa ahadi zote.

Alisema pamoja na kuingia udhamini timu ikiwa chini kwenye msimamo, lakini iliweza kuamsha morali na kuweza kumaliza kwa mafanikio na kwamba ameridhishwa na matokeo.

“Japo tulitamani nafasi nne za juu ili tushiriki kimataifa, lakini nilifurahishwa na matokeo na wiki ijayo nitakuwa na kikao cha wazi na nitalipa kila kitu” alisema na kuongeza

“Nimeshaelekeza viongozi wafanye tathimini ili kile nilichoahidi nitalipa na mkataba nitaongeza kwa ajili ya msimu ujao, tunahitaji usajili bora ili ushindani tulioonesha uendelee” alisema Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Mbeya.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Tanzania Prisons, Ajabu Kifukwe alisema watafanya tathmini hiyo ili wanapoenda katika kikao hicho wawe na ripoti iliyoshiba.

“Sisi tupo tayari na tunasubiri kikao hicho, tutafanya tathimini mapema ili tuwe na ripoti iliyoshiba, kimsingi tunatarajia kuanza mapema mipango ya msimu ujao” alisema Kifuke.