Mbunge apeleka mashabiki 120 kuisapoti Pamba Shinyanga

Muktasari:

  • Pamba Jiji FC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ikiwa na pointi sita sawa na vinara Mbeya City ingawa inazidiwa kwa utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika kuhakikisha Pamba Jiji FC inaibuka na ushindi ugenini dhidi ya Stand United, Septemba 22 kwenye mechi ya Ligi ya Championship itakayochezwa katika Uwanja wa Kambarage, Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula ameahidi kugharamia usafiri wa mashabiki 120 wa timu yake kwenda kuisapoti katika mechi hiyo.

Pamba imeanza vyema mechi mbili za mwanzo za Ligi ya Champioship ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Cosmopolitan na kisha ikapata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pan African jambo lililoifanya iwe nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo.

Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula

Mabula alisema anatambua mchango wa mashabiki katika kufanikisha ushindi wa Pamba Jiji FC hivyo atawasapoti kwa kugharamia usafiri wa kwenda na kurudi Shinyanga.

"Natambua tarehe 22 timu inakwenda kucheza Shinyanga na Stand United. Nitoe rai kwa mashabiki wote, mimi kama mbunge nikiwa mwakilishi wa wananchi na mpenda michezo, natumia nafasi hii kuwahakikishia mashabiki wasiopungua 120 tutapata usafiri kutoka hapa kwenda Shinyanga na kurudi.

"Tunachohitaji ni hamasa kwenye timu yetu. Tukatoe hamasa, shangwe na sapoti kwa timu yetu dakika ya kwanza hadi ya mwisho. Kila tutakuwa tunaenda maeneo haya tutahakikisha tunafanya jitihada, mashabiki sapoti tuhakikishe tunafanya vizuri," alisema Mabula.

Mabula alisema mwamko wa mashabiki mkoani Mwanza unatoa ishara ya wazi kuwa watafanya vizuri msimu huu na kupanda Ligi Kuu.

"Nitoe shukrani zangu nyingi kwa mashabiki wa mpira wa Mwanza kwa namna ya kipekee walivyoipokea timu yetu ya Pamba Jiji FC. Morali imekuwa kubwa na hamasa ni kubwa.

"Tumeona mechi ya kwanza matokeo ni mazuri sana. Mechi ya pili ilikuwa ngumu lakini tumepata ushindi. Alkadhalika ndivyo inavyotakiwa kuendelea kuhakikisha tunashinda kila mechi iwe nyumbani au ugenini," alisema Mabula.