Mayanga: Hii vita ni kali, lakini natoboa

Tuesday November 23 2021
mayanga pic
By Damian Masyenene

HADI sasa straika wa Polisi Tanzania, Vitalis Mayanga ndiye kinara kwenye orodha ya wafungaji bora baada ya kuweka mabao manne kwenye michezo sita waliyocheza hadi sasa.

Mayanga ambaye licha ya kutovuma, lakini amekuwa na mwenendo mzuri tangu alipoanza soka lake la ushindani alipokuwa akikipiga Stand United ‘Chama la Wana’ kwa misimu minne mfululizo kuanzia 2015.

Itakumbukwa msimu wa 2018/19 alikuwa mfungaji bora katika kikosi cha Ndanda FC akifunga mabao 10 na kuzitamanisha Simba na Yanga wakitaka huduma yake kutokana na kazi yake nzuri uwanjani.

Straika huyo amekuwa mtamu msimu huu kutokana na kiwango bora anachoonesha uwanjani, huku pia akiisaidia zaidi timu yake kuwa ndani ya nafasi tatu za juu kwa pointi 10 wakiachwa alama moja na bingwa mtetezi Simba.

Kutokana na matokeo waliyonayo katika timu, lakini kasi yake aliyoanza nayo imemuibua na kutamka kuwa msimu huu lazima atoboe licha ya vita kali iliyopo.

Anasema hatua ya kuongoza kwenye ufungaji bora kwa sasa inampa nguvu na matumaini ya kuweza kujiingiza kwenye king’anyiro cha kuwania tuzo ya ufungaji bora.

Advertisement

Anaongeza kuwa hata suala la timu yake kuwa katika nafasi nzuri inaongeza chachu kwa wachezaji kuendelea kupambana kuhakikisha hawashuki nafasi tatu za juu.

“Ushindani ni mkali lakini nashukuru kwa mwanzo mzuri na Mungu akijalia naweza kutoboa, kimsingi ni kuendelea kupambana kuisaidia timu na mimi mwenyewe,” anasema Mayanga.

Anafafanua kuwa mipango yake ni kuendelea kufunga kadri ya uwezo wake na anavyopata nafasi huku akiwashukuru wenzake kikosini kumpa ushirikiano.

Anasema kuwa malengo ya timu ni kuona wanafanya vizuri wakipambana kila mechi kusaka alama tatu na kwamba mwanzo walioanza nao unatia matumaini.

“Kama timu ina mipango yake, tunahitaji kila mechi kupata pointi tatu, tunaelewa ushindani uliopo lakini hatuwezi kuogopa au kukata tamaa, isipokuwa ni kuongeza juhudi,” anasema Mayanga.

Kocha mkongwe hapa nchini, Meja mstaafu Abdul Mingange anasema Mayanga amekuwa na kiwango bora kwa nyakati zote na kwamba anashangaa kuona hata Taifa Stars hawamuoni.

Anasema straika huyo ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo mkubwa na kama watapewa nafasi na kuaminiwa hata kwenye majukumu ya Taifa anaweza kusaidia kitu.

Anabainisha kuwa kwa muda aliomuangalia nyota huyo, amebaini kuwa na kitu ndani na kama ni ishu ya kufunga mabao, staa huyo anaweza kuwa msaada hapa nchini.

“Huwa nashangaa kuachwa kwa Mayanga kuitwa kwenye kikosi cha Taifa, nimemfuatilia muda mrefu amekuwa na kiwango bora ambapo akipewa nafasi anaweza kutupa kitu cha ziada,” anasema Mingange.

Advertisement