Mawakili wa Salehe waomba kuondoa kesi mahakamani

Muktasari:

  • Salehe ni miongoni mwa wagombea urais wa TFF walioenguliwa kwenye usaili kwa kutokidhi takwa la kikanuni la kuwa na wadhamini angalau kuanzia watano.

Jaji Edwin Kakolaki ametumia dakika 45 kusikiliza kesi namba 98 ya kupinga katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania  (TFF) kabla ya mawakili wa upande wa mashtaka kuiomba Mahakama Kuu Dar es Salaam kuiondoa kesi hiyo na kufungua upya.

Kesi hiyo iliyofunguliwa na Ally Salehe aliyeenguliwa kuwania urais wa TFF ilitajwa leo mahakani hapo ikiwa ni siku kadhaa baada ya kesi ndogo namba 305 ya kutaka kusitisha mchakato wa uchaguzi wa TFF kama ilivyoombwa na Salehe kutupiliwa mbali.

Jaji Kakolaki alisema haoni sababu za msingi za kusitisha uchaguzi na atatoa hukumu ya kesi ya msingi kabla ya uchaguzi wa TFF wa Agosti 7.

Hata leo mawakili wa Salehe wameomba kuiondoa mahakamani kesi hiyo kwani kuna taarifa ambazo hawakuziweka mwanzo.

"Mahakama imeridhia tuiondoe na kisha tutaifungua upya," amesema Frank Chacha mmoja wa mawakili wawili wa Salehe waliojitokeza mahakamani leo.

Amesema kesi hiyo ilipotajwa Julai 16, walipewa amri kufanya masahihisho kwenye faili lao.

"Baada ya kusanya taarifa ya mteja wetu tumeona marekebisho tu haitoshi, hivyo tumeomba kuiondoa na kisha tutairudisha tena mahakamani na mahakama imekubali na kututaka ndani ya siku 14 tuwe tumekwishakuleta madai mapya,".

Amesema awali kuna
Kuna hoja ambazo hawakuzipata tangu mwanzo kwa ajili ya kesi hiyo.

"Huu ni utaratibu tu wa kisheria kwa kuwa kuna taarifa mpya ambazo hatukuzipata mwanzo hivyo  tumeomba kuiondoa kwanza," amesema.

Amefafanua kwamba hata kama uchaguzi utafanyika kabla ya kesi yao ya msingi kutolewa hukumu, kwenye kesi yao ikibainika kulikuwa na makosa kisheria kwa viongozi waliochaguliwa wataenguliwa.