Mastaa walioanza Messi akiichezea Barcelona mechi ya kwanza

Muktasari:
- Messi ametoka mbali katika soka. Leo tunakikumbuka kikosi cha kwanza cha Barcelona wakati Messi alipoichezea Barca kwa mara ya kwanza Oktoba 16, 2004.
CATALUNYA, HISPANIA.DUNIA ya soka imeendelea kushuhudia uhodari wa hali ya juu wa staa wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi anayetajwa kuwa mwanasoka bora wa muda wote duniani.
Juzi katika pambano dhidi ya Real Betis ugenini, mashabiki wa Betis walilazimika kumshangilia Messi licha ya kuichapa timu yao Hat Trick katika ushindi wa mabao 4-1.
Messi ametoka mbali katika soka. Leo tunakikumbuka kikosi cha kwanza cha Barcelona wakati Messi alipoichezea Barca kwa mara ya kwanza Oktoba 16, 2004.
Victor Valdes
Huyu ndiye aliyekuwa langoni katika pambano hili la kwanza la Messi katika kikosi cha wakubwa dhidi ya Espanyol. Valdes aliendelea kuwa kipa wa kwanza wa Barcelona mpaka mwaka 2014 wakati alipoondoka kwenda Manchester United.
Maisha yake Old Trafford hayakwenda sawa kama alivyopanga. Baadaye akatimkia katika timu ya Middlesbrough, pia alishindwa kurudi katika ubora wake. Aliondoka Middlesbrough msimu wa 2016/17 na baada ya kukaa bila ya timu hatimaye Valdes alitangaza rasmi kustaafu soka Januari 2018. Kwa sasa ana umri wa miaka 38.
Juliano Baletti
Mlinzi wa kulia wa Barcelona siku hiyo. Baada ya hapo aliichezea Barcelona na kuifungia Barcelona bao katika pambano la fainali Ligi ya mabingwa wa Ulaya dhidi ya Arsenal mwaka 2005. Miaka miwili baadaye aliondoka Barcelona na kutimkia Chelsea mwaka 2007 ambayo alitwaa nayo ubingwa wa Ligi Kuu England, pia mataji mawili ya FA. Staa huyu wa kimataifa wa Brazil alistaafu soka mwaka 2011 ikiwa ni siku 12 tu baada ya kusaini mkataba na klabu ya Ceara ya kwao Brazil. kwa sasa ana umri wa miaka 42.
Oleguar Preasas
Mlinzi wa KIdachi ambaye hakuacha jina kubwa sana Nou Camp. Wakati Messi akicheza mechi yake ya kwanza Barcelona, Preasas alikuwa mlinzi wa kati katika safu ya ulinzi ya Barcelona akishirikiana na mkongwe, Carles Puyol. Preasas alikuwa amekulia katika shule ya soka ya Barcelona mpaka kupandishwa kikosi cha wakubwa. Mwaka 2008 alijiunga na Ajax ambayo aliichezea kwa miaka mitatu mpaka alipoachana na soka.
Anajulikana kwa kupenda mambo ya siasa na mwaka 2010 alijiunga na kundi la waandamanaji jijini Amsterdam kwa sababu za kisiasa. Ana umri wa miaka 39 kwa sasa.
Carles Puyol
Mlinzi mkongwe wa Barcelona ambaye alimwona Messi tangu siku ya kwanza alipotua Barcelona. Aliichezea Barcelona kwa miaka yake yote ya soka mpaka alipostaafu soka mwaka 2014. Mpaka sasa anajishughulisha na soka akiwa na kampuni yake ya uwakala wa wachezaji.
Mlinzi wa Borussia Dortmund, Marc Bartra ni miongoni mwa wateja wake.
Giovanni Van Bronckhrost
Alicheza upande wa kushoto siku hiyo. Alikuwa amehamia Barcelona msimu mmoja tu uliopita akitokea Arsenal.
Baada ya miaka mitatu tangu awe katika kikosi hiki alirudi kwao kukipiga katika klabu ya Feyenoord. Kwa sasa amekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo na misimu miwili iliyopita alitwaa kombe la KNVB (FA ya Uholanzi) katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo.
Rafael Marquez
Mlinzi wa kati wa Mexico ambaye alikuwa na kipaji kikubwa. Mpaka miaka miwili iliyopita alikuwa nahodha wa Mexico akiwa na umri wa miaka 37. Aliondoka Barcelona mwaka 2010 na kuanzia hapo alianza kuzurura katika klabu za New York Red Bulls, León, Hellas Verona na sasa anakipiga katika klabu ya Atlas ya kwao Mexico. Ana umri wa miaka 40 kwa sasa.
Deco/Messi
Katika pambano hili kiungo mahiri wa kimataifa wa Ureno mwenye asili ya Brazil ndiye ambaye alitengeneza historia kwa kumpisha Messi aingie uwanjani katika dakika ya 83 ya pambano hili dhidi ya Espanyol. Baadaye Deco alitimkia Chelsea kabla ya kurudi kwao Brazil kukipiga katika klabu ya Fluminense. Aliachana na soka mwaka 2013 nyuma yake akiacha Sub ya kukumbukwa zaidi katika soka.
Xavi Hernandez
Yupo katika siku za mwisho za usakataji wa soka nchini Qatari akikipiga katika klabu ya Al Sadd. Ameacha jina kubwa nyuma yake na anakumbukwa kwa kutengeneza utatu mtakatifu uwanjani. Yeye, Andres Iniesta na Lionel Messi. aliondoka Barcelona mwaka 2015 na mpaka sasa akiwa na umri wa miaka 39 anakipiga Qatari ingawa anaweza kustaafu soka muda wowote kuanzia sasa.
Ronaldinho
Inaaminika kuondoka kwa Ronaldinho Barcelona kwa kiasi kikubwa kulichangiwa na kuibuka kwa Messi. Mpaka leo jezi yake namba 10 ndio ambayo inavaliwa na Messi. aliondoka Barcelona mwaka 2018 na kutimkia AC Milan. Baada ya hapo alizurura huku na kule ikiwemo kucheza kwao Brazil kabla hajastaafu soka rasmi Januari mwaka jana.
Henrik Larsson
Staa wa kimataifa wa Sweden. Alicheza Barcelona kwa misimu miwili na bado alifanikiwa kutwaa mataji mawili ya La Liga pamoja na ubingwa wa Ulaya wa mwaka 2006. Aliondoka Barcelona baada ya kutwaa ubingwa huo mwaka 2016 na kurudi kwao kukipiga katika klabu ya Helsingborg kabla ya Manchester United kumchukua kwa mkopo wa muda mfupi.
Baadaye alirudi kwao Sweden na kustaafu soka kabla ya kuwa kocha wa klabu yake ya Helsingborg. Baadaye aliachana na klabu hiyo baada ya yeye na mwanae kushambuliwa uwanjani na mashabiki. Kwa sasa ni kocha msaidizi wa klabu ya Angelholm hapo hapo Sweden.
Samuel Eto’o
Tangu aondoke Barcelona mwaka 2009 akipisha kizazi cha Messi, staa huyu wa kimataifa wa Cameroon amecheza katika nchi za Italia, Russia na England. kwa sasa anakipiga katika klabu ya Qatari SC ya Qatari baada ya kupitia katika klabu ya Antalyaspor ya Uturuki. Ana umri wa miaka 38.
Andres atokea katika benchi
Kama ilivyo kwa Messi, katika pambano hili dhidi ya Espanyol, mkongwe mwingine wa Barcelona, Andres Iniesta naye alitokea katika benchi kuingia uwanjani. Iniesta, ambaye anaingia katika kundi la wachezaji wachache duniani ambao hawajawahi kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia kwa sasa anakipiga Japan.