Mastaa Simba kuoga mahela

Sunday October 24 2021
mastaa pic
By Clezencia Tryphone

MASHABIKI wa Simba wameitwa uwanjani Benjamin Mkapa huku wakipewa tahadhari mapema ili kuepuka kuiponza klabu yao, huku mabosi wa klabu hiyo wakiwahakikisha mastaa wao kuwa wataendelea kuoga noti kama kawaida iwapo watapambana na kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba leo inaikaribisha Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mchezo wa marudiano huku ikiwa na faida ya mabao 2-0 ilioupata ugenini wiki iliyopita, lakini Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likitoa nafasi ya watazamaji 15,000 tu kuingia Kwa Mkapa.

Kutokana na idadi hiyo, ambayo ni robo ya mashabiki 60,000 wanaoingia Kwa Mkapa, uongozi wa Simba umetoa tahadhari kuwataka mashabiki wazingatie agizo hilo ili wasiingie matatani kama watani wao Yanga waliolimwa fainai ya Sh 11 milioni kwa kutodhibiti mashabiki wao walipovaana na Rivers United.

Tuanze na ishu ya noti. Mastaa wa Simba wamehakikishiwa na mabosi wao kwamba bonasi ya kila wanaposhinda mechi zao iwe za kimataifa ama za ligi ya ndani ipo pale pale, licha ya kwamba bilionea wao, Mohammed ‘Mo’ Dewji, alijiengua uenyekiti wa bodi ndani ya klabu hiyo.

Simba imekuwa na kawaida ya kuwapa motisha wachezaji wao ili waweze kufanya vizuri na kutimiza malengo ya klabu ambayo wamejiwekea katika michuano husika ambapo hutenga Sh150-300 milioni endapo timu ikishinda, bonasi ambazo hutegemea na aina ya timu waliyoifunga.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliyechukua nafasi ya Mo, alisema bonasi zao zipo kama kawaida na kwamba mastaa hao, kazi ipo kwao kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwenye kila mchezo ukiwamo wa kesho dhidi ya Galaxy.

Advertisement

Try Again alisema, kila kitu ndani ya klabu hiyo kinaenda sawa na kama ilivyokuwa msimu uliopita timu ikishinda na kutoka sare kuna bonasi ambazo nyota wao wanapata na wanalifahamu hilo.

“Simba ni taasisi, kila kitu kinaenda kama kilivyokuwa hapo nyuma, hakuna kilichobadilika hata kidogo, hata bonasi zipo na zitaendelea kuwepo, wachezaji wetu tunawaamini sana kwa kupambana,” alisema Try Again.

Kuhusu mechi ya kesho dhidi ya Galaxy, Try Again, alikiri itakuwa na ushindani mkubwa kuliko hata watu wanavyofikiria, kwani anaamini wapinzani wao watashuka uwanjani ili kutaka kulipa kisasi baada ya kupoteza nyumbani kwao.

Alisema ni mchezo wa tahadhari kubwa licha ya kwamba rekodi yao kwenye uwanja wa nyumbani inawabeba.

Simba haijapoteza mechi ya Ligi ya Mabingwa kwenye uwanja wa nyumbani kwa miaka nane sasa, sawa na miezi 104 au wiki 453, tangu mara ya mwisho ilipolala 1-0 dhidi ya Recreativo do Libolo ya Angola Februari 17, 2013 kwenye Uwanja wa Taifa.

Try Again alisema wamejiandaa kupambana kulinda rekodi yao nzuri nyumbani na kutinga hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo.

“Tulishinda kwao hata wao wanaweza kushinda kwetu ndio mpira ulivyo, tumejiandaa kiakili kupambana tusipoteze, tusonge mbele,” alisema.


AONYA MASHABIKI

Kuhusu Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kutoa nafasi ya mashabiki 15,000 alisema hilo ni moja ya jambo kubwa ambalo wanatakiwa kujivunia na kuingia uwanjani kwa kufuata taratibu zaidi za wataalamu wa afya.

“Nawaomba mashabiki wetu waje uwanjani na tahadhari kubwa sana, wavae barakoa, wanawe mikono na kukaa umbali mtu mmoja baada ya mwingine, tuepuke kupewa adhabu, fursa hii ni kubwa kwetu, tunawashukuru sana CAF na TFF,” alisema Try Again akirejea kilichowakuta Yanga katika mechi yao ya raundi ya awali dhidi ya Rivers United na kujikuta wakitozwa faini ya Dola 5,000 (zaidi ya Sh11 milioni) kwa kuruhusu mashabiki na pia kufanya fujo kwa maofisa wa timu pinzani.

Kipa wa zamani wa kimataifa, Ivo Mapunda aliwataka nyota Simba kuingia uwanjani kwa tahadhari kwa kuwa bado hakuna mwenye uhakika wa kusonga mbele licha ya kuongoza mabao 2-0.

Mapunda, aliyezidakia Prisons, Simba, Yanga Moro United na Taifa Stars na kucheza nje ya nchi alisema nyota wa Simba wanatakiwa kuingia kwa tahadhari kubwa itakayowapa matokeo mazuri na kusonga hatua inayofuata.

Alisema wana kila sababu ya kutoboa kwani chama lao lina kikosi bora na kusisitiza hata bonasi wanayowekewa mezani ni moja ya njia ya kuwaongezea mzuka zaidi wa kuiua Galaxy.

Advertisement