Masoud ana mawili Chama la Wana

Muktasari:
- Sare ya Stand United ya bao 1-1, dhidi ya Polisi Tanzania, imeifanya timu hiyo kujihakikishia nafasi ya kucheza mechi za mtoano 'Play-Off', kusaka tena tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao, baada ya kufikisha pointi 60.
BAADA ya Stand United 'Chama la Wana', kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao moja kwa moja, kocha wa timu hiyo, Juma Masoud amesema kwa sasa ana kazi kubwa ya kupambania maeneo mawili muhimu, beki na ushambuliaji.
Sare ya Stand United ya bao 1-1, dhidi ya Polisi Tanzania, imeifanya timu hiyo kujihakikishia nafasi ya kucheza mechi za mtoano 'Play-Off', kusaka tena tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao, baada ya kufikisha pointi 60.
Stand iliyoshuka daraja msimu wa 2018-2019, inawania nafasi hiyo dhidi ya Geita Gold iliyoshuka msimu uliopita na tayari itamaliza nafasi nne za juu, kwani pointi zake 55, ilizonazo hazitofikiwa na timu yoyote.
Akizungumza na Mwanaspoti, Masoud alisema katika mechi za hivi karibuni, washambuliaji wa kikosi hicho wamekosa utulivu wa kumalizia nafasi, sawa na eneo lote la beki ambalo linafanya makosa ya kujirudia, jambo analopambana nalo kwa sasa.
"Sababu ya kudondosha pointi zilizotunyima nafasi ya kupanda Ligi Kuu moja kwa moja ni kutokana na presha kubwa iliyopo kwa wachezaji, walijiamini kupitiliza mno ndiyo maana wakajikuta wanafanya makosa mengi yasiyokuwa na msingi," alisema.