Mashabiki Simba waridhishwa na kiwango cha timu

Muktasari:

  • Kikosi cha Simba kimepoteza kwa bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki kunogesha kilele cha tamasha la Simba Day.

LICHA ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe, baadhi ya mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi Simba jijini Mwanza wameonyesha kuridhishwa na kiwango cha timu yao huku wakiwa na matumaini kibao kuwa kitafanya vizuri msimu huu na kubeba mataji kama kawaida.

Wakizungumza na Mwanaspoti baada ya kumalizika mchezo huo usiku huu baadhi ya mashabiki hao wamesema hawana wasiwasi kwani kiwango cha timu yao na wachezaji wapya ni cha kuotea mbali.

Mmoja wa mashabiki hao, Ramadhan Pomo mkazi wa Kiloleli amewataja Sadio Kanoute,Pape Osmane Sakho na Peter Banda kama nyota wapya waliotisha katika mchezo huo.

Naye Ramadhan Prudence amesema uwezo uliooneshwa na timu yake ni wa kuridhishwa na unatia matumaini huku akituma salamu kwa watani wao Yanga kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii Jumamosi Septemba 25, mwaka huu wajiandae kushushiwa kichapo.

Mwenyekiti wa Simba tawi la Kiloleli, Deus Yassin amesema nidhamu ya timu katika kukaba na kushambulia ni nzuri ambapo amewataka mashabiki kutulia na kukiamini kikosi chao.