Manyasi azigonganisha Singida BS, Mtibwa Sugar

Muktasari:
- Miongoni mwa hizo ni Mtibwa Sugar iliyopanda daraja na Singida Black Stars inayohitaji nguvu mpya kuelekea michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika - zote zimejikuta zikitua kwa kiungo wa Kagera Sugar, Geofrey Manyasi.
BAADA ya msimu wa Ligi Kuu Bara kukamilika Juni 25, mwaka huu, timu zimeanza mipango ya kuimarisha vikosi kwa ajili ya msimu ujao ikiwemo kusajili wachezaji wapya na kuboresha maeneo yenye upungufu.
Miongoni mwa hizo ni Mtibwa Sugar iliyopanda daraja na Singida Black Stars inayohitaji nguvu mpya kuelekea michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika - zote zimejikuta zikitua kwa kiungo wa Kagera Sugar, Geofrey Manyasi.
Manyasi ambaye amemaliza mkataba wa mwaka mmoja na Kagera Sugar iliyoshuka daraja msimu huu, amelithibitishia Mwanaspoti kutafutwa na klabu hizo pamoja na KMC, huku akisisitiza kuwa bado anapitia ofa zote tatu ili kufanya uamuzi.
Kiungo huyo aliyewahi kutamba na Boma, Geita Gold, Tanzania Prisons na Pamba, alisema anafurahia maisha ya likizo huku akisubiri msimu kuanza na kujua timu atakayoitumikia Ligi Kuu msimu ujao.
“Baada ya kumalizana na Kagera Sugar mipango iliyopo sasa kuna timu zinanihitaji baadhi ndiyo nasikilizia hapa. Nimefuatwa na KMC, Mtibwa Sugar na Singida Black Stars. Kitu muhimu zaidi ni makubaliano yawe mazuri maana timu za Bongo ni zile zile,” alisema.
“Mimi siangalii sana suala la uhakika wa namba maana najua nikipambana mazoezini basi nitacheza kwani najua nini kimenileta kwenye timu nitakayokuwepo, lakini najua mambo ya maslahi yanazungumzika.”
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti hivi karibuni, kiungo mkabaji wa Pamba Jiji ya Mwanza, James Mwashinga alimtaja Manyasi kuwa mmoja ya viungo wanaofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara na anapenda kujifunza kwake.