Mandonga: Chakula cha buku hadi tv kila chumba

Muktasari:

  • Mandonga atamaliza adhabu hiyo iliyotokana na kusimamishwa kupanda ulingoni na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), kufuatia kupokea kipigo cha TKO ya raundi sita dhidi ya bondia mkongwe, Mada Maugo mwezi uliopita mjini Morogoro.

MEI 12, mwaka huu bondia wa ngumi za kulipwa nchini na mpiga debe wa zamani wa Kituo cha Mabasi Msamvu mjini Morogoro, Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’ atakuwa akimaliza adhabu yake.

Mandonga atamaliza adhabu hiyo iliyotokana na kusimamishwa kupanda ulingoni na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), kufuatia kupokea kipigo cha TKO ya raundi sita dhidi ya bondia mkongwe, Mada Maugo mwezi uliopita mjini Morogoro.

Bondia huyo nyota yake ya umaarufu iling’ara zaidi 2022 baada ya kuchapwa na Christopher Magambo licha ya tambo zake hasa ile ya ‘Mandonga Mtu Kazi’ na ‘Ukipigwa Ndonga Utalalaâ’ ambapo mwisho wa siku alilala yeye kwa KO ya raundi ya kwanza.

Safari ya umaarufu wake ilizidi kuwa kubwa na kuanza kusahau maisha ya kupiga debe katika Stendi ya Msamvu baada ya kutakiwa na kupanda ulingoni kupambana na Shaban Kaoneka.

Hapa ndipo mashabiki wa ngumi na wasiokuwa mashabiki wa mchezo huo walianza kumjua zaidi Mandonga kwa mikwara ambayo alimchimba Kaoneka kama ule “Kaoneka umeyakanyaga” au ule “Umepanda mtumbwi wa Vibwengo” na badala yake akaupanda mwenyewe kwa kupigwa katika pambano hilo. Ipo misemo mingi ya Mandonga aliyojipambanua nayo kwa kuwatishia wapinzani wake ukiwemo Ngumi ya Pelesupelesu akimaanisha ngumi inayokata kona na Ngumi Ndoige. Mandonga mwenye rekodi ya kupanda ulingoni kwenye mapambano 14 akiwa ameshinda sita kati ya hayo matatu kwa KO, amepigwa mara tano kati ya hayo manne ni kwa KO, huku sare zikiwa mbili.

Mandonga amefanya mahojiano maalum na Mwanaspoti na kueleza mambo mengi yaliyomo ndani ya mchezo huo na maisha yake nje ya ngumi.

Bondia huyo ameanza kwa kufichua mambo ambayo yalimfanya kuwa kimya kwa muda mrefu kabla ya kupanda ulingoni mwezi uliopita katika pambano alilopoteza. Katika mahojiano na Mwanaspoti bondia huyo amefunguka mambo mengi na mipango kibao iliyopo mbele yake, lakini akigusia pia maisha ya zamani ya kula mlo wa buku na sasa akiwa na uwezo wa kuingia hotelini na kuagiza chakula cha Sh15,000 akalipa bila wasiwasi. “Ukimya wangu nadhani Mungu mwenyewe alichangia kwa sababu nimepigana sana tena katika kipindi cha muda mfupi. Kwa hiyo ikafikia wakati Mungu amenipa nafasi ya kupumzika katika ngumi ili kukusanya nguvu,” anasema Mandonga.

“Namshukuru Mungu, nimeingia msituni na nimetoka kwa mara nyingine tena kwa hiyo najua Watanzania wenzangu watapata burudani nyingi na watafurahi zaidi kama Mandonga ‘Mtu Kazi’ amerudi.”

SWALI: Umerudi na mguu mbaya maana umetoka kupigwa na Maugo, nini kilichangia kupoteza?

JIBU: “Nilipoteza raundi ya sita ila kwangu naona haikuwa bahati yangu siku ile kushinda lakini namshukuru Mungu kuweza kumaliza pambano salama na hata walipotoa matokeo kuwa Maugo ameshinda, sikushanga kwa sababu najua kwamba wakati wa Mungu ni wakati sahihi na haikuwa na sababu kubwa ya kuweka malalamiko, nilikubaliana na mchezo na nijipange na mchezo mwingine.

SWALI: Umefahamika zaidi kama bondia aliyetokea kupiga debe lakini kuna taarifa uliwahi kuwa mwanasoka, ipoje hiyo? JIBU: “Nimepitia michezo mingi hadi kufikia hapa kabla ya kucheza soka nilikuwa mwanamuziki na nilikuwa densa, nimecheza sana bolingo yaani nilikuwa densa mkubwa Mkoa wa Morogoro.

“Lakini ilifikia wakati nikaachana na muziki, nikaingia katika soka, tulikuwa na timu yetu pale stendi ilikuwa inaitwa Msamvu Terminal ‘Mpira Pesa’ yaani goli moja dola mia.

“Baadaye niliachana na mambo ya mpira na kuingia kwenye mchezo wa  ngumi, namshukuru Mungu kwa jinsi anavyonielekeza siyo kubaya maana kila ninapokwenda napata riziki yangu.

SWALI: Pesa ya kwanza kuishika ilikuwa kiasi gani? JIBU: “Unajua katika utafutaji wa pesa Mungu huwa ndiyo anapanga, pesa yangu niliyopata haikuwa kwenye ngumi, nilishawahi kushika Sh21 milioni kwa sababu nilikuwa na miradi yangu mwenyewe.

SWALI: Miradi gani wakati kazi yako ilikuwa kupiga debe?

JIBU:“Nilikuwa na mradi wangu na ulisifika sana Morogoro. Nilikuwa na biashara ya kuchoma tofali yaani nawafyatulisha watu tofali halafu naweka matanuri ya matofauli kwa ajili ya kuchoma na nilikuwa nauza kila tofali shilingi 100 kwa kibao cha nchi tatu.

SWALI: Watu wengi wanajua umekuja kwenye ngumi ukiwa umechoka ukitokea kwenye debe lakini?

JIBU: Unajua sijawahi kuwa na majigambo kwamba nina kitu fulani au nafanya jambo fulani ila mtu akifika nyumbani kwangu Morogoro, wewe (mwandishi) umeshawahi kufika katika mahojiano mengine na familia yangu, ambaye hajawahi kufika akija nitamuonyesha matanuri ya matofali niliyokuwa nachoma.

“Nilikuwa nimeajiri watu 24 ambao kazi yao ilikuwa kufyatua tofali za Mandonga, nilikuwa na muda wa kuja stendi kupambana halafu siku tatu nasema naumwa kumbe napambania mradi wangu.

“Lakini nilikuwa sikai sana kwenye tofali kwa sababu nina kaka yangu alikuwa akisimamia anaitwa Shida ingawa nilikuwa namuita sana Ndonga Moko. Katika upande wa ngumi imekuwa tofauti kwa sababu nimepata matunda makubwa ambayo sikuwahi kuyashika, ridhiki zilifuatana na Mungu akanifungulia milango mpaka kumiliki magari.

“Nimeweza sasa kumiliki nyumba na siyo moja, ninazo mbili Morogoro, moja ipo Mkambarani katika eneo la ekari moja na nusu na nyingine ambayo nilianza kuijenga mwaka 2004 kabla ya ngumi, ilitokana na kazi yangu ya tofali ila ngumi imeniongezea pesa kubwa nashukuru Mungu kwa hilo.

“Nadhani kama binadamu wangekuwa wanapinga kama jambo hili siyo zuri basi naamini nisingekuwa na nafasi kubwa kwangu ila nashukuru Mungu mimi Mandonga nimekuwa miongoni mwa wanaotazamwa zaidi Tanzania katika ngumi.

SWALI: Kitu gani unakimisi wakati ule wewe ni mpiga debe na sasa kwenye ngumi?

JIBU: “Kitu kikubwa ambacho huwa nakikumbuka ni watu niliokuwa nao katika utafutaji pale Msamvu, wapo ndugu na rafiki zangu na nikiwa Morogoro huwa napita kuwasalimu.

“Lakini nje ya hapo hakuna ninachokumbuka na hakuna tajiri anayekumbuka shida kwa sababu ukishapata njia kubadilisha maisha yako huwezi kung’ang’ania tena kwenye shida zako ulipotokea.

“Kule kunabaki kama kumbukumbu sasa nitakumbuka vitu vipya ambavyo vimenishangaza kama nilikuwa natembea kwa miguu sasa natembelea gari, kama nilikuwa naenda hotelini kula kwa Sh1,000 kwa sasa ninaweza kuingia hotelini na kula Sh15,000 hadi 20000. Namshukuru Mungu kwa fursa aliyonipa na anaendelea kunipa.”

SWALI: Kwa nini mkeo hatumuoni kwenye ngumi?

JIBU: “Ngumi siyo mchezo rafiki sana kama hujaukubali kwenye moyo wako ila kwangu mimi siyo kwamba shemeji yako (mkewe) hajawahi kuonekana.

“Shemeji yako ameshawahi kuonekana kwenye ngumi lakini mwenyewe huwa hapendi kuja kwenye mchezo wa ngumi, kipindi nacheza na Christopher Magambo napigwa raundi ya kwanza alikuwepo ukumbini. Yeye mwenyewe anajua mume wake ni mpiganaji, siku ile hakuwa na wasiwasi, asilete vitu vya ubabaishaji maana anajua nitaendelea kuwa mpiganaji na nikipoteza nitajipanga upya.

SWALI: Hajawahi kukwambia uache ngumi?

JIBU: “Binafsi hajawahi kuniambia niache ngumi kwa sababu yeye mwenyewe ameona yalivyobadilisha maisha yetu kutokana na mchezo wa ngumi, sasa hivi anaangalia screen mbilimbili. Akitaka kitu cha baridi anafungua jokofu, akitaka kupika sasa anawasha jiko la gesi lile la sahani tatu, akifanya taa, limewaka tofauti na hapo itakuwa ni uongo kwa mke wangu kuniambia mchezo wa ngumi niache.

“Sasa hivi ukija kwangu kuna runinga hadi ya wageni ambayo ina chumba chao maalum siyo sebuleni.

“Unajua mafanikio haya ni kama yamechelewa, lakini mabondia wote wa hapa nchini unawaowajua mimi ndiyo mkubwa wao kiumri ila naonekana mdogo kuliko wao.

SWALI: Kitu gani kilikubeba baada kupigwa na Magambo kiasi cha watu kukufuatilia?

JIBU: “Namshukuru Mungu kwa kuwa mchezo nimeupenda kutoka moyoni lakini mabondia wengi katika mchezo huu huwa wakihojiwa wanajitamba sana ila akienda kwenye pambano akapigwa akifuatwa kuhojiwa tena huwa anashindwa kuzungumza kama ilivyokuwa mwanzo.

“Sasa mimi Mungu amenipa kipaji cha pekee, bondia yeyote wa Tanzania hajapata na ndiyo maana nikawaambia kwamba ukinipiga kama nimekupiga na nikikupiga nimekupiga tu. Nikimaanisha kwamba mimi hata ukinipiga huwa nina nguvu ya kufanya mahojiano ambapo naelezea mchezo ulivyokuwa nikiwaambia mashabiki wangu au watazamaji kilichotokea, lakini ikitokea nimekupiga basi nakuwa nimekupiga zaidi. Hiyo ndiyo nafasi ambayo nimeipata, namshukuru Mungu maana hata yule Magambo Christopher alivyonipiga hakuwa na maneno mengi ila nikampiga nje ya ulingo katika mahojiano na vyombo vya habari, nilimpiga raundi ya pili, nikabaki mjini Mandonga Mtu Kazi.

SWALI: Lakini Shaban Kaoneka alikubeba zaidi?

JIBU: “Shaban Kaoneka siyo alinibeba, nilijibeba mwenyewe kwa sababu na Mungu alinipokea, nikiongelea lile pambano la Songea nilitengeneza tangazo kubwa lakini Kaoneka aliacha mchezo wa ngumi baada ya kupigwa na Kidunda (Seleman) ambaye alikuwa akijiita Mtu Kazi zamani. Sasa hilo jina tulikuwa tunagombea mimi na yeye (Kidunda) aliniachia baadaye akajiita Nusu Mtu Nusu Jini.

“Lakini nikirudi kwa Kaoneka yeye alisema kabisa baada kupigwa kwamba ameacha ngumi anarudi kulea familia yake ila tangazo langu wakati ule ndiyo likawa limemrudisha mjini.

“Suala la mimi kupanda sana ilikuwa ni jambo la Watanzania kutokea kunipenda kwa vile nilivyokuwa nayakubali matokeo niliyokuwa nayapata tena kwa spidi ileile ambayo nilianza nayo awali.

“Baada ya pambano lile ndiyo nilianza kupokea simu nyingi kutoka Dar, nilitoka Songea na gari ya jeshi ambayo ilikuwa imechukua mabondia wa jeshi hadi Dar na hapo ikawa safari kujuana na watu wengi.

ITAENDELEA KESHO