Manara: Hans Poppe ameacha pengo kubwa kwa mpira wetu na Simba

Msemaji mpya wa Yanga, Haji Manara ametumia post tatu kwenye akaunti yake ya Instagram kumuelezea aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Zakaria Hans Poppe.

Hans Poppe alifariki dunia jana usiku katika hospitali ya Aga Khan. Manara amemzungumzia kama mmoja ya watu wake wa karibu sio tu kikazi bali kifamilia. Ameandika;

"Nimechelewa sana kusikia taarifa za huu msiba wa mzee wetu Zakaria, Imenifadhaisha sana na imeniondolea mood yangu.
Kwangu alikuwa mwanamichezo halisi shupavu na ameacha pengo kubwa kwa mpira wetu na klabu yake kwa ujumla,"

"Kutoka kwenye kinywa chake mwenyewe nilimjua vema Captain kama nilivyopenda kumwita kwa jina hilo siku zote,
licha ya kutembeleana mara kwa mara, nimesafiri nae mara nyingi mno kwa gari yake kwenda mikoani kwenye mechi za Ligi,"

"Ni mjuzi wa hadithi za maisha na kiukweli alikuwa na hadithi nyingi tamu, moja ya hadithi tamu ninayoifikiria kuiandikia hata kitabu ni vita ya Kagera ambayo Captain alipigana na ile sakata la kesi yao,"

"Alinihadithia pia kuhusu jinsi yeye alivyofanikiwa kuwa mfanyabiashara mkubwa baada ya miaka mingi ya kuishi gerezani. Hakika Captain Zacharia alikuwa ni Chuo kamili kwa waliomfahamu na mjuzi wa dunia na ishtighali zake. Unajua nini ,licha ya kuwa mkristo lakini anaweza kusoma Suraat Yaasin nzima bila kuangalia mahali. Usilolijua kuhusu yeye pia ni fundi wa kucharaza gitaa la solo na kwenye uvulana wake akiwa mdogo alishiriki kiasi na bendi ya Safari Trippers kama Mwanamuziki akiwa na Marehemu Marijani Rajabu,"