Maftah amuuma sikio Tshabalala

BEKI wa zamani wa kushoto wa kimataifa aliyewahi kuwika na Yanga, Simba na Taifa Stars, Amir Maftah amemuuma sikio beki na nahodha msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kama kuna timu imetokea yenye mkwanja inayomhitaji ni vyema akasepa tu.

Mkataba wa Tshabalala unaisha mwishoni mwa msimu huu na klabu kadhaa ikiwemo Kiazer Chief ya Afrika Kusini zinahitaji huduma yake na inaelezwa mabosi wa Simba wameamua kumzuia kwa kumwekewa Sh300 milioni mezani ili asiondoke.

Kwa miaka tisa ambayo Tshabalala ameitumikia Simba tangu alipojiunga nayo ametoa mchango kwa  kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara nne, mataji mawili ya ASFC, kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili tofauti na robo nyingine ya Kombe la Shirikisho.

Akizungumza jijini hapa, Maftah alisema katika maisha fursa huwa haiji mara mbili na kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kunamfanya mchezaji azidi kujifunza mambo mengi.

“Hata mimi niliondoka ndio akapata nafasi yeye sasa na yeye kama imekuja ofa nzuri kutoka timu nyingine anangoja nini kuondoka, haya ni maisha baadae watu wanakuja kuanza kukucheka eti kisa ulikuwa na upendo na timu,” alisema beki huyo wa zamani.

Katika hatua nyingine beki huyo ambaye amewahi kuichezea timu ya Taifa ‘Taifa  Stars’ alisema nchi kwa sasa inapitia wakati mgumu kutokana na kutokuwepo kwa beki wa kushoto mzawa mwenye uwezo kama enzi zao.

“Tshabalala na wengine ndio wanaondoka wengine wapo wapi?,kuna wakati unaona hadi David Luhende anaitwa timu ya Taifa hakuna beki wa kushoto,” alisema beki huyo wa zamani

Hata hivyo, anashauri iwekwe misingi madhubuti katika soka la vijana ili kuzalisha  mabeki wa kushoto wenye uwezo kama ilivyokuwa wao.