Madhara ya mchezaji kukwatuliwa mara nyingi

Muktasari:

  • Pasipo kujua kuwa maneno kama hayo anapoyasikia mhusika huwa ni mwiba unaochoma, lakini kwa wachezaji wanaocheza mara kwa mara hukumbana na kadhia ya kukwatuliwa na wachezaji pinzani.

Huwa ni kawaida mashabiki au watazamaji wa soka kuwa wepesi wa kulaumu pale wanapoona mchezaji anacheza soka laini au kwa woga uwanjani.

Ni kawaida lawama hizo kumlenga zaidi mchezaji ambaye ni staa wa timu husika.

Pasipo kujua kuwa maneno kama hayo anapoyasikia mhusika huwa ni mwiba unaochoma, lakini kwa wachezaji wanaocheza mara kwa mara hukumbana na kadhia ya kukwatuliwa na wachezaji pinzani.

Wengi hawajui kuwa mchezo wa soka una magumu yake wakati wa kucheza hali inayochangia kwa wachezaji kulazimika kubadili mbinu za kiuchezaji.

Soka ni mchezo mgumu unaohusisha matumizi ya nguvu na kasi, huku pia mpinzani akikabana naye jambo ambalo linahusisha kukumbana kimwili.

Uchezaji wa soka na nafasi wanazocheza wanasoka unawaweka katika hatari ya kupata majeraha yatokanayo na michezo. Ingawa zipo mbinu za kukwepa majeraha lakini mchezo wa soka ni ngumu kukosa majeraha.

Wachezaji ambao wanaongoza mara kwa mara kukwatuliwa ni wale wanaocheza eneo la katikati kama vile viungo na washambuliaji na wale wanaocheza nafasi za pembeni kama vile mawinga na mabeki wanaopanda kushambulia.

Nafasi kama hizo hukumbana na kukwatuliwa mara kwa mara kutoka kwa wapinzani wao na hii ni kutokana na mtindo wa uchezaji unaohusisha kushambulia kwa kukimbia kwa kasi, kupiga chenga na kukabana.

Hivi karibuni imesikika klabu ya Arsenal na wale watangazaji wa soka Ligi Kuu England wa televisheni wakionya kuhusu mchezaji Bukayo Saka kutokana na kukwatuliwa mara nyingi.

Ni kweli ukitazama mechi nyingi za Ligi Kuu England za Arsenal utakubaliana na hilo kuwa mchezaji huyo katika kila mechi hukumbana na kukwatuliwa mara kwa mara.

Hii ndio ilichangia kwa Klabu ya Arsenal kutoa angalizo kwa marefa kumlinda mchezaji huyo kinda dhidi ya kukwatuliwa na mabeki na viungo kutoka kwa wachezaji wa timu pinzani.

Hata kwa waliotazama mchezo wa jana wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Buyern Munich wanaweza kuona namna mchezaji kinda kama huyu anavyokumbana na mabeki wa timu pinzani.

Marefa wanapigiwa kelele kuwalinda kwa kuwa wakali na kuwaadhibu wale mabeki wote wanaocheza rafu mbaya za kupania,  za makusudi na zisizo na uungwana katika soka.

Wilfred Zaka aliyekuwa anacheza Crystal Palace ambaye sasa anacheza nchini Uturuki katika timu ya Galatasaray ndiye mwanasoka anayeshika namba moja kwa kukwatuliwa kuliko mwanasoka yeyote duniani.

Mchezaji huyo mpaka sasa amekwatuliwa mara 685 katika mechi kubwa alizocheza soka la kimataifa katika ligi kubwa duniani.

Siyo pekee katika ligi hizo, hata katika Ligi Kuu Bara wapo wachezaji wa nafasi za ushambuliaji ambao wanakutana na kadhia ya kukwatulia mara kwa mara.

Na ni kawaida kwa mashabiki kukasirika pale beki anapopitwa kirahisi na winga au mshambuliaji. Kwa shabiki huweza kupiga kelele za kumtaka beki huyo kutokubali na ikibidi amkwatue winga huyo ili asilete hatari kwa timu yao.

Mtakumbuka enzi za winga machachari Edibily Lunyamila wakati akiwa katika kiwango cha juu na mmoja wa mawinga bora kuwahi kutokea nchini, naye alikuwa akikumbana na kukwatuliwa mara kwa mara.

Hii ilitokana na uhodari wake wa kukimbia kwa kasi na kuwapiga chenga mabeki na kutoa krosi zenye kuleta faida katika timu yake. Hivyo utaona kuwa uhatari wake katika eneo analocheza linamfanya kuchungwa kwa kila namna na mabeki na ikibidi hukwatuliwa.

Kwa kukwatuliwa mara kwa mara ambapo washambuliaji au mawinga huwa wanapaniwa na wachezaji pinzani, ndiko ambako kulichangia mchezaji kama Eden Hazard kupata majeraha mara kwa mara hatimaye kulazimika kuachana na soka angali bado akiwa na uwezo mkubwa mguuni. Pamoja na mwili kuwa na ustahimilivu wa majeraha ya kila siku wanayopata, lakini pale mwili unapozidiwa na majeraha husababisha madhara mbalimbali ya kimwili na kiakili.

MADHARA YALIVYO

Madhara ambayo anayapata mwanasoka kwa kukwatuliwa mara kwa mara ni kupata majeraha makubwa katika misuli, nyuzi ngumu za tendoni na ligamenti na pia kuteguka na mivunjiko ya mifupa.

Majeraha hayo yanachangia wanasoka wa aina hii kupata majeraha makubwa ambayo yanawaweka nje muda mrefu ili kupisha muda wa kuunga vizuri.

Maumivu sugu na uvimbe, kutokana na kuchezewa faulu mara kwa mara wanasoka hawa hujikuta wakipata majeraha na vijimichubuko katika miili ambavyo huwapa maumivu sugu ya muda mrefu.

Wakati mwingine wanasoka hao hujikuta wakiwa watumwa wa kutumia dawa za maumivu kwani baadhi huweza kujinunulia wenyewe pasipo kushauriwa na daktari.

Matumizi holela ya dawa za maumivu nayo huweza kuchangia kupata majeraha ya mara kwa mara au kutokupona kwa wakati.

Vilevile kuna ulemavu wa kudumu. Kitendo cha kukwatuliwa mara kwa mara humfanya mchezaji kupata majeraha eneo fulani la mwili ikiwamo hasa katika goti na kifundo cha mguu.

Kujeruhiwa kwa nyuzi ngumu za ligamenti huwasababishia wanasoka kuwa na matatizo ya kudumu ya goti au kifundo cha mguu. Hii huchangia pia ulemavu wa kudumu katika goti.

Ukiacha madhara ya mwili, wachezaji wanaopata madhara ya kukwatuliwa na kuwa nje muda mrefu hupatwa na matatizo ya kiakili ikiwamo kuumia kihisia, msongo wa mawazo na sonona. Jaribu kufikiria mchezaji anaachana soka sababu ya majeraha ya mara kwa mara angali bado ana umri mdogo na bado kiwango chake kipo juu.

Kutokana soka kuwaingizia kipato kikubwa na kuwa ajira kwao wanapokuwa nje kutokana na majeraha hupata matatizo ya kiakili kutokana na kuwaza mambo mengi.

Mchezaji anapofahamu kuwa anapaniwa mara kwa mara na kukwatuliwa na kuumizwa hupatwa na hali ya woga au hofu kiasi cha kushindwa kucheza vizuri.