Lwanga: Tutakomaa mpaka kieleweke

Wednesday April 07 2021
Lwanga pc
By Oliver Albert

KIUNGO wa Simba, Taddeo Lwanga amefurahishwa na jinsi timu yake ilivyotinga kibabe kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini amesema wanatakiwa kuwa fiti na kupambana kwa asilimia 200 hatua inayofuata ili kutimiza malengo yao ya kufika Fainali.

Simba imetinga hatua hiyo baada ya kuichapa AS Vita ya DR Congo mabao 4-1 hivyo kuongoza kundi A ikiwa na pointi 13 na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Al Ahly utakaofanyika Ijumaa nchini Misri.

Lwanga aliyesajiliwa Simba wakati wa dirisha dogo la usajili, Desemba mwaka jana ameonyesha kiwango kikubwa kwenye mashindano hayo na hata katika ligi hivyo kuwavutia mashabiki wa klabu hiyo ambao wameanza kusahau utawala wa mzawa Jonas Mkude.

Lwanga amekiri kuwa wamepambana sana mpaka kufikia hatua hiyo lakini wanatakiwa kuongeza juhudi zaidi hatua zinazofuata ili kuweka rekodi mpya kwenye mashindano hayo.

“Tunafurahi kuwa tumefanikiwa kufanya kile tulichokipanga. Kufika robo fainali kunatokana na ushirikiano mkubwa wa kila mmojac.

“Vita ni timu kubwa lakini tumewafunga kutokana na morali ya kila mmoja hivyo tutahakikisha kuwa mechi ya mwisho (dhidi ya Al Ahly) nayo tunapata matokeo mazuri licha ya kwamba sio kazi rahisi,” alisema Lwanga.

Advertisement

Akizungumzia kuhusu hatua waliyofika, Lwanga alisema wanatakiwa kujiongeza zaidi na kucheza kwa asilimia 200 ili kufikia malengo yao ya kucheza fainali ya michuano hiyo.

“Huko tunakokwenda kila timu ni ngumu hivyo tunatakiwa kuongeza bidii zaidi na kucheza si kwa asilimia 100 ila kwa asilimia 200 ili kuweza kutimiza malengo yetu ya kufika fainali na naamini Mungu atatusaidia,” alisema.

Advertisement