Lipo la kuchukua Simba mafanikio Ligi ya Mabingwa

KUANZIA juzi saa moja jioni unaweza kumwambia lolote shabiki wa Simba akafurahi. Kila utakachosema kizuri katika timu atakubaliana nawe hata ukiisema vibaya timu yake hatakuwa mkali - atakucheka tu. Ndio. Ana furaha na klabu yake katika ushindi wa juzi dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Simba iliifunga Ahly katika mchezo wao wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa bao 1-0 wakiwa nyumbani, na sasa wanaongoza kundi lao wakiwa juu haya yakiwa mapinduzi makubwa katika kipindi cha misimu mitatu.

Simba sio tu waliwafunga Ahly, lakini pia walicheza vyema katika mchezo huo - waliupiga mpira mwingi na kuwabana Waarabu hao ambao wana rekodi kubwa sio tu Afrika, bali hata duniani ikiwa ndio moja ya klabu yenye mataji mengi.

Simba ilitawala na kuwapa wakati mgumu Ahly, lakini pia usisahau Waarabu hawa walikuwa na kocha mwenye rekodi bora Afrika, Pitso Mosimane ambaye tangu atue katika klabu hiyo hakuwahi kupoteza na mchezo huu unakuwa wa kwanza kupoteza katika mashindano ya ndani ya Afrika.

Hebu tuangalie Simba imeshindaje kwa mara ya pili mfululizo mbele ya Ahly hapa nyumbani kwani sio kitu ambacho kimekuwa kikizoeleka kutokea, lakini wekundu hawa zama hizi wamefanikiwa kukifanya na wakakithibitisha bila shaka.

Swali hili sio sisi tunaweza kujiuliza, bali hata wao Ahly lazima watoke wakajifungie kisha kujiuliza mara mbili imekuwaje kila wanapoingia Tanzania wanaangukia wapi yaani wanakosea au wapi wale Simba wamefanikiwa kuwashika na kuwapa wakati mgumu kiasi hicho.

Hapa nchini inawezekana wapo ambao wanaweza kuchukia au hata kuona kwamba Simba imebahatisha au haikustahili, lakini binafsi naona yapo ambayo klabu zetu zingine hasa Yanga na hata Azam ambazo zimekuwa na ushiriki wa mashindano ya Afrika kujifunza kutoka Simba wakiwa katika mechi za kibabe kama hizi.

Eneo la kwanza lazima klabu zijifunze kuwa na utulivu katika mipango ya kushinda mechi zao. Klabu nyingi hazina viongozi wanaojua kukubaliana kwamba hebu tutengeneze mkakati wa kutafuta ushindi na klabu nyingi zinaongozwa na watu wengi ambao sio waaminifu kwa klabu zao.

Ukishakuwa na mkakati wa ushindi lakini ndani yake wakaibuka wachache ambao wakawa si waadilifu na zaidi wakapoteza uaminifu sio rahisi kuonja mafanikio kama haya ambayo Simba wanayapata sasa. Viongozi wao wanahitaji pongezi ya kwamba wakiwa ndani wanajipanga kisha wakitoka na mkakati waliokubaliana kama hawatatimiza kwa asilimia 100, basi hata asilimia 90 watatimiza yale ambayo wanataka kuyafanya.

Ukiacha usafi wa viongozi wao lakini pia wachezaji wao wamekuwa wakishika kile ambacho wanakisikia kutoka kwa viongozi wao. Simba imekuwa ikisisitiza - tena bila woga kwamba Ahly hawatatoka, lakini pia wachezaji wao wamevaa ile jihadi kwamba wakiwa nyumbani hakuna anayetoka. Safari iliyopita tuliona na tukakosoa kwamba ile kauli yao kwamba nyumbani hatatoka mtu na kweli hakuna aliyetoka kama ilivyo sasa kuwa iliwafanya kutofanya vizuri ugenini, lakini sasa tumeona wamebadilika na Simba hata ugenini ambako ilichapwa mabao 5-0 safari hii wamechukua pointi tatu.

Ukiangalia hata mchezo wa juzi utagundua kwamba wachezaji wa Simba ni ‘wanajeshi watiifu’ ambao walipambana kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya mwisho hawakuwa na sababu ya kuwahofia Ahly ambao waliwaona kama wako sawa nao, lakini kikubwa ni kile kujiaminisha kwamba hakuna anayetakiwa kuwafunga wakiwa nyumbani.

Klabu zingine zimekuwa tofauti. Zimekuwa rahisi sana kupoteza nyumbani wakati mwingine katika akili ya ndogo sina maana kwamba hakuna klabu ambayo imeifunga Ahly hapa, zipo kuna Yanga kama ambavyo ilifanya mwaka 2014 lakini jihadi ya namna hii lazima iambukizwe kwa klabu ili ziwe na damu kama ya Simba. Mwisho ni mashabiki wao ambao muda wote wa mchezo walikuwa nyuma ya wachezaji wao waliwapa nguvu.