Mwakalebela awaachie wengine waizungumzie klabu

MIONGONI mwa viongozi wanaoonekana kupenda kuzungumza na vyombo vya habari hasa kwenye mambo ya kutetea klabu ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela.

Wakati Simba hawajabadili mfumo wa uendeshaji na kutoka wanachama kwenda kampuni, basi kulikuwa na viongozi ambao pia walipenda kutolea ufafanuzi kwa kila jambo.

Ashukuriwe Mungu hivi sasa ndani ya Simba kuna utaratibu maalumu wa kutoa habari huku Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ akipiga marufuku kwa mjumbe yeyote kuzungumza na vyombo vya habari.

Mo huenda aliona mbali kwani kuna baadhi ya viongozi ndani ya klabu hiyo naweza kusema walikuwa waropokaji na sio wazungumzaji maana walikuwa hawaangalii ni jambo gani la kuzungumza kwenye vyombo vya habari na kwa wakati gani.

Viongozi hao hawakujali madhara yanayoweza kutokea kwa klabu mara baada ya kumaliza kutoa taarifa zao, hilo Mo Dewji alilishinda, amewadhibiti hasa kama ni taarifa basi utazipata ila zitakuwa ni taarifa za ndani tu.

Yanga sasa huwezi kumsikia Mwenyekiti wao, Dk Mshindo Msolla akizungumza na vyombo vya habari ila anapaswa sasa kuwaelekeza watendaji wake wengine kuangalia ni taarifa gani ya kuitolea ufafanuzi ama nani atolee ufafanuzi wa taarifa husika.

Ni mara kadhaa taarifa ya Yanga ikitolewa na Mwakalebela basi ni lazima itazua mkanganyiko kwa wadau wa michezo kama ilivyokuwa hivi karibuni alipokuwa akielezea malalamiko yake juu ya waamuzi kwenye mechi zao za Ligi Kuu Bara.

Baada ya kutoa kauli hiyo iliyotafrisiwa kwamba endapo Yanga wangepoteza dhidi ya Mtibwa Sugar basi wangejitoa kwenye ligi, kila kona ilizungumzwa kwamba Mwakalebela sasa anastahili kupumzika kuzungumzia masuala ya klabu maana anaharibu.

Ni kweli inawezekana kila mmoja alitafsiri kwa namna anavyoelewa lakini ukiona kwamba hata wanachama wenyewe wa Yanga wanalalamikia kauli za kiongozi wao ujue kwamba kuna shida sehemu.

Kwanza inaelezwa kwamba mara nyingi kiongozi huyo hupewa jukumu la kuzungumzia masuala ya malalamiko tu ama ambayo yanaonekana kutokuwa sawa ndani ya Yanga wakikumbusha ishu ya Bernard Morrison alipotua Simba.

Kwenye sakata la Morrison, Mwakalebela e alikuwa kama mstari wa mbele kuipigania klabu yake lakini alionekana kama amekwenda tofauti kwa namna ambavyo lilipokelewa na mashabiki wa soka huku wakikumbuka mambo kadhaa yaliyowahi kutamkwa na kiongozi huyo.

Wakati mwingine Mwakalebela amekuwa kama akishindana na Haji Manara ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Simba ambaye kumkera mtu ni kitu cha kawaida kwake lakini inakuwa tofauti na pale anapozungumzia kiongozi huyo.

Hiyo huenda linatokana na nafasi yake ndani ya klabu na pengine nyazifa ambazo amewahi kuzishika kwenye soka, hivyo huonekana ni kiongozi anayependa kulalamika sana.

Hakuna anayepinga kuelezea malalamiko yake lakini cha kujiuliza ni kwamba Yanga kuna watendaji ambao wanaweza kuyazungumzia hayo pale tu wanapopewa maelekezo ya kwenda kutolea fafanuzi wa jambo fulani.

Lakini kwasababu tu Mwakalebela ameonekana kutoleweka vizuri anapowasilisha jambo lake basi ni vyema akawapa nafasi wengine wawe wanazungumza mambo ya klabu.

Mwakalebela sasa afanye mambo mengine ambayo hayatahusiana na malalamiko ama kuelezea jambo linaloonekana kuwa na utata, maana kuna mawili, moja huenda anashikwa na jazba ama anawasilisha vibaya na kuonekana ni kiongozi tofauti mwnye mrengo tofauti na malengo ya klabu.

Hakuna asiyefahamu utendaji kazi wa Mwakalebela tangu akiwa Mtibwa Sugar hadi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) tena chini ya kiongozi bora kabisa Leodger Tenga

Kaka yangu, inaonekana watu hawajakuelewa na hawataki kukuelewa kabisa, sasa jivue kwenye majukumu mengine yenye utata pengine unakuwa unazungumza kwa hisia ama maumivu makali hadi kufikia hatua watu hawaelewi unawasilisha nini.

Una maumivu makubwa na madai ya Yanga kuonewa, lakini hawaelewi ikiwemo wanachama wenu wanaodai kuwa unaongea sana pasipo kueleweka, wape wengine wawasilishe ili hali ya hewa isichafuke ndani ya klabu yenu.