Kwa Yanga hii, mtaumia

Wednesday April 07 2021
Yanga pc
By Khatimu Naheka
By Clezencia Tryphone

NYOTA wa Yanga wako siriaz kambini wakipambana na hali yao na sasa wanatifuana kujiandaa na muendelezo wa ligi lakini kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi ametoa kauli ya matumaini.

Mastaa wa Yanga wamezidi kumkosha Mwambusi wakijiandaa kujumuika na Sebastian Migne ambaye ndiye Kocha Mkuu ajaye. Kiufundi wamebadilika katika kutengeneza nafasi na hata kufunga.

Yanga ilikuwa na shida kubwa ya kutengeneza nafasi katika michezo yake kadhaa iliyopita na hata wakitengeneza kuzitumia inakuwa shida hatua ambayo ilileta ugumu katika mechi zao na kusababisha hata makocha kutimuliwa.

Akizungumzia maboresho ya kikosi chake, Mwambusi ameliambia Mwanaspoti kwamba, ameona mabadiliko makubwa kwa wachezaji wake namna ambavyo wanashambulia na kutengeneza nafasi.

“Timu imeimarika sana, nimeona kupitia mchezo wa Jumamosi waliokutana wenyewe kwa wenyewe, naona kuna kitu kikubwa kimebadilika sana kwa timu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mbeya City, Prisons, Moro United na Azam.

yANGA PCC
Advertisement

Mwambusi ambaye anasifika kwa misimamo mikali ya kinidhamu alisema; “Changamoto ya kutengeneza nafasi na kumaliza ilikuwa ni kubwa sana ila wachezaji wote ni wazuri sana na wanafaa kutwaa ubingwa wa Ligi.”

Aidha, Mwambusi ambaye ni mkali wa mazoezi ya fiziki, aliongeza kuwa kuna wachezaji watatu wa timu ya vijana ambao amewapandisha timu kubwa kuzidi kuwajenga zaidi.

Lengo kubwa la kuwapa ndisha nyota hao Mwambusi anasema ni kwa ajili ya kuwajenga na kuwapa nafasi ya kujiamini ili huko usoni waweze kuisaidia Yanga.

“Kwa kutambua thamani na umuhimu wa vijana ndio maana nawapa nafasi wacheze na hawa kaka zao wazoefu ili huko usoni tusipate shida ya kufanya usajili, tunakuwa nao wa kwetu tu na kuwapa nafasi,” alisema na kusisitiza anataka soka la kushambulia.

Kocha huyo alisema kila mchezaji ili apate nafasi anatakiwa kutumia vyema kila dakika atakayopewa uwanjani lakini pia kumshawishi kwa kujituma mazoezini. “Nikiwaambia mnionyeshe nani ana uhakika wa namba hapa hilo litakuwa gumu kila mmoja ana nafasi ya kucheza kwa kuwa kila mmoja namuona yuko sawa.”

Advertisement