Kubenea atinga TFF kuchukua fomu ya urais, ang'aka

Muktasari:

Mpaka leo saa 8 mchana wagombea tisa wamejitokeza kuwania urais wa TFF kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 7 mjini Tanga.

Mbunge wa zamani wa Ubungo, Said Kubenea amechukua fomu ya urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) huku aking'aka kucheleweshwa.

Kubenea ametinga TFF saa 7:45 mchana akiwa ameambatana na mtu mwingine mmoja na kuongoza kuingia kwenye ofisi ya mwanasheria wa TFF.

Hata hivyo alitakiwa kusubiri hadi saa 8:00 kwa kuwa mtoaji fomu amekwenda kula, jambo ambalo lilimkera na kuhoji sababu ya ofisi hiyo kufungwa.

"Nimekuja kuchukua fomu ya kugombea urais, niko na wadhamini wangu kutoka mikoani wanapaswa kunidhamini ili warudi mikoani, lakini mtoaji fomu hayupo," aling'aka Kubenea.

"Huwezi kufunga ofisi, hii ni taasisi ya Umma, huu ni uchaguzi hivyo maofisa wanaoshughulikia uchaguzi wawe zaidi ya mmoja ili mwingine akitoka wengine wanaendelea na kazi, kinachofanyika hapa ni ukiritimba ilikutuchelewesha ila tutakomaa hadi kieleweke," amesema.

Baada ya kuchukua fomu, Kubenea amesema amemchukulia Ally Salehe ambaye ni wakala wa kimataifa wa wachezaji anayetambulika na Fifa.