Mwanamke ajitosa kumvaa Karia urais TFF

Muktasari:

Uchaguzi mkuu wa TFF utafanyika Agosti 7 jijini Tanga na kesho Jumamosi ndio mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu.

Wakati joto la uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likizidi kupanda, Hawa Mniga amekuwa mwanamke wa kwanza kuchukua fomu ya kuwania urais wa shirikisho hilo.

Hawa amechukua fomu hiyo ili kupambana rais wa TFF anayemaliza muda wake, Wallace Karia ambaye alichukua fomu ya kuwania tena nafasi hiyo Juni 8.

Mwanamke huyo ambaye ni mtumishi wa umma, alifika ofisi za  TFF  leo Ijumaa saa 11:00 asubuhi kisha kuingia moja kwa moja ndani kuchukua fomu.

Baada ya nusu saa alitoka lakini akagoma kuzungumza lolote kwa madai sio muda wa kampeni na kisha kuondoka eneo hilo.

Hawa ni mdau mkubwa wa soka na amewahi kuwa katika kamati ya ajira ya TFF.

Hadi sasa idadi ya waliochukua fomu ya urais imefika nane huku wengine wakiwa ni Karia, Deogratius Mutungi, Ally Mayay, Evans Mgeusa, Oscar Oscar, Tarimba Abbas na Zahir Mohammed Haji.

Pia kwenye nafasi ya ujumbe, hadi kufikia saa 5 asubuhi jana waliochukua fomu walikuwa ni Athuman Kambi, Lameck Nyambaya, Liston Katabazi, Michael Petro na Sandy Mohammed 'Kimji' ambao wanawania nafasi hiyo kutoka kanda namba moja inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro na Pwani wakati kutoka kanda namba 2 yenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga waliochukua fomu ni Khalid Abdallah Mohammed.

Kutoka Kanda namba 4 yenye mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Simiyu na Singida waliochukua fomu ni Mohammed Aden na Osuri Kosuri huku Kanda namba 5 inayojumuisha mikoa ya Geita, Kagera, Mwanza na Mara ni Salum Umande Chama pekee aliyechukukua fomu hadi kufikia muda huo.