KMC yaipchapa Kagera Sugar

MCHEZO kati ya KMC na Kagera Sugar umemalizika pale uwanja wa Uhuru huku  KMC imeibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Mchezo huo ulioanza saa 8:00 mchana ulishuhudiwa KMC ikiwa bora zaidi katika dakika zote 45 za kipindi cha kwanza ikifanikiwa kupiga mashuti manne yaliyo lenga lao na moja kati ya hilo lilikuwa ni goli lililofungwa na Abdul  Hillal dakika ya 16.

Kagera ilishindwa kuifungua safu ya ulinzi ya KMC inayoongozwa na Andrew Vicent na Lusajo Mwaikenda.

Katika dakika zote za kipindi cha kwanza ilifanikiwa kupiga mashuti mawili yaliyolenga lango na ili kushiria kwamba haikufika kabisa kwenye lango la KMC haijaotea hata mara moja.

Mipira mingi ya Kagera iliishia kwa Abdallah Masoud anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji na akafanya kazi kubwa kuhakikisha ni hatari chache zinazowakuta mabeki wake wa kati.

KMC inatumia zaidi eneo la pembeni kupandisha mashambulizi jambo linaloonekana kuifungua zaidi safu ya ulinzi ya Kagera.

Kipindi cha pili kilianza kama kipindi cha kwanza kilivyoisha kwa KMC  kulisakama zaidi lango la Kagera na dakika ya 63 ilifanikiwa kukwamisha mpira wavuni kupitia kwa Matheo Antony, Lakini mshika kibendera namba moja akanyoosha kibendera kuashiria kuwa ni Offside.

Kagera ilifanya mabadiliko katika kipindi cha pili kwa kumuingiza Jackson Kibirinde na KMC ikamtoa Charles Ilanfya na kumuingiza Hassan Kabunda.

Kuanzia dakika ya 65 hadi 70,  Kagera ilimiliki mpira zaidi  lakini kuanzia dakika ya 71o makali yaliisha na KMC ikarudisha umiliki wake.

Dakika ya 77, baada ya kumiliki sana mpira Hassan Kabunda aliipatia KMC bao la pili kwa shuti alilopiga mara tu baada ya kuingia kwenye boksi la Kagera.

Dakika chache baadae Kabunda alipiga shuti kali nje ya boksi la Kagera lililomshinda golikipa na kuiandikia KMC bao la tatu.

Kosa kosa za hapa na pale zilizompa shida golikipa wa Kagera Said Kipao ziliendelea lakini hadi dakika 90 zinamalizika ubao ulikuwa unasomeka 3-0.

Baada ya mchezo huo KMC imefikisha alama 31 sawa na kuishusha Ruvu Shooting kwenye nafasi ya tano, wakati Kagera imeendela kusalia nafasi ya tisa kwa alama 24.

Kocha wa Kagera Mecky Maxime alizungumzia mchezo huo akisema:"Tumetoka kucheza mechi ngumu dhidi ya Yanga na tulitumia nguvu  nyingi,  ukiangalia leo tumecheza saa nane na unajua mchezaji unapocheza kwenye jua kali kama lile hali lazima itakua ngumu, ingawa siwezi kutumia hiki kama kisingizio."

Kwa upande wake kocha wa KMC, John Simkoko amesema:"ulikuwa mchezo mzuri na mbali ya kwamba tumeshinda, lakini tumecheza mpira wa kuburudisha."