Dida: Ihefu inabaki ligi kuu tunakaza msuli

Muktasari:

Ihefu imeendelea kujikongoja, imetoka mkiani na sasa ipo nafasi ya 16, jambo linalompa imani kipa Deogratius Munishi 'Dida' kwamba watabaki, kikubwa wanakaza msuri

KIPA wa Ihefu, Deogratius Munishi amesema mzunguko wa pili una mahesabu makali unaomfanya kila mchezaji kufikiria jinsi ya kukamilisha malengo ya klabu iliomuajiri, ili kulinda uaminifu.

Amesema kutokana na timu yake kuwa kwenye wakati mgumu, anapambana kadri awezavyo kuhakikisha anafanya kitu chakuisaidia  timu kusalia kwenye ligi kuu msimu ujao.

"Kazi ya soka sio nyepesi kama mchezaji hataichukua kwa uzito wa kujitolea akili yake nguvu na muda ili  kutimiza malengo ya timu anayoichezea, kutokana na ushindani ulivyo mgumu mzunguko wa pili kila mchezaji anatakiwa kukaza msuri,"amesema.

Amesema hawezi kukata tamaa kwasababu alijiunga na Ihefu kupitia usajili wa dirisha dogo ikiwa inaburuza mkia na sasa ipo nafasi ya 16, jambo linalompa imani ya timu hizo kupanda nafasi za juu zaidi.

"Sio kazi nyepesi lakini kila mchezaji ajitoe kwa kadri awezavyo, naamini tukiendelea kuhamasishana tutafika mbali na tutamaliza msimu kwa furaha" amesema.

Ihefu imecheza michezo 20, imeshinda nne, imetoka sare tano, imefungwa 11, kupitia matokeo hayo imevuna pointi 17.