Kisinda, Saido watema cheche unaambiwa

Saturday May 08 2021
kisinda pic
By Mwandishi Wetu

MASTAA wawili wa Yanga winga Tuisila Kisinda na mshambuliaji mkongwe Said Ntibazonkiza ‘Saido’ wametoa kauli mbili ambazo kama mabeki wa Simba watazisikia zitawapandisha presha kuelekea mechi ya leo ya watani.

Kwanza walichofanya Yanga kupitia matajiri wao wa GSM ni kama kuwapa mzuka wachezaji wawili Wakongomani Kisinda na Mukoko Tonombe wakimalizana nao kwa fungu dogo la usajili tena kabla ya muda waliokubaliana kufika.

Hatua hiyo ikamfanya winga huyo kuongeza gia mpya kuelekea mchezo huo wa watani na sasa kafungua mdomo akifungukia maandalizi yake.

Aliyeanza ni Kisinda ambaye Simba lazima watakuwa wanajiandaa kukabiliana na kasi yake akisema wala mechi hiyo haimpi presha na sasa yupo timamu.

Kisinda alisema anatambua itakuwa mechi ngumu, lakini kucheza kwake mchezo huo mara ya pili kumempa mzuka wa kujua anatakiwa kufanya kipi katika dakika 90.

“Sasa niko sawa kabisa kiafya na kimchezo, tunaendelea na maandalizi ya mwishomwisho, najua tunakwenda kucheza mechi ngumu lakini kwa sasa sina presha yoyote kuelekea mchezo huo,” alisema Kisinda.

Advertisement

“Ile mechi ya kwanza kidogo nilikuwa nataka kujua inakuwa ni mechi ya aina gani, lakini mchezo huu hautakuwa na presha yoyote kwangu, muhimu ni kuwa katika ubora wangu niweze kuisadia timu yangu.”

Kisinda aliongeza kuwa ana shauku ya kucheza mechi kubwa kama hizo ambazo zimekuwa zikitambulisha zaidi makali yake.

“Nilipokuwa DR Congo wananijua inapokuja tunacheza na Mazembe, huwa napenda kung’aa katika mechi za namna hii, lakini nataka kufanya kazi kubwa zaidi katika mechi hii kuliko nilivyocheza mechi ya mbili zilizopita,” alisema.


MSIKIE SAIDO

Alichosema Saido kwa upande wake ni maneno mafupi tu kwamba wakati wakiwa katika maandalizi ya mwisho kila kitu kipo sawa na kwamba kwa sasa wanasubiri muda wa mchezo tu.

“Tuko sawasawa hii ni mechi kubwa hapa nilicheza moja kule Zanzibar lakini hii inakuwa muhimu zaidi kwa ajili ya ligi, tunawaheshumu wapinzani wetu lakini sio kuwaogopa, maandalizi tuliyofanya ni mazuri na yanatupa hamasa muhimu sasa ni kusubiri tu muda wa mchezo,” alisema.


VIGOGO KAMBINI

Juzi jioni wakati kikosi hicho kikiendelea na mazoezi vigogo kutoka upande wa uongozi wakiongozwa na mwenyekiti wa klabu, Dk Mshindo Msola, Senzo Mazingisa na wajumbe wa kamati ya utendaji wakiambatana pia na mkurugezi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said walitua mazoezini.

Vigogo hao walishuhudia mazoezi hayo wakati kocha Nesreddine Nabi akiendelea kupanga silaha zake, kisha baada ya mazoezi wakapata futari pamoja na kikosi na dua nzito kufanyika.

Vigogo hao waliwaambia wachezaji ujio wao kambini hapo ilikuwa kuangalia maandalizi yanavyoendelea, lakini kutakuwa na kikao rasmi cha kutoa ahadi yao ya ushindi ambayo itawashtua wote.

Advertisement