Prime
Kisa Simba, Yanga Lawi aitwa mezani

Muktasari:
Mwanaspoti katika kutaka kujiridhisha zaidi iliamua kumtafuta katibu wa timu hiyo, Omary Ayoub ambapo alipoulizwa alisema hayo ni mambo yao ya siri na asingeweza kuyaweka hadharani kwa sasa.
BEKI wa kati na nahodha wa timu ya taifa ya vijana U20, Ngorongoro Heroes. Lameck Lawi, leo atakuwa uwanjani huko Misri, ili kukamilisha ratiba ya hatua ya makundi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon U20), huku timu hiyo ikiwa imeshaaga michuano, lakini huku nyumbani kuna kitu kilichokuwa kinaendelea.
Mabosi wa Coastal Union, klabu anayoichezea walianzisha mazungumzo naye ili kumuongezea mkataba mpya kuhofia vigogo, Simba na Yanga visimbebe bure baada ya awali kuvigomea kwenye madirisha mwili ya usajili yaliyopita katika Ligi Kuu Bara.
Simba na Yanga zimekuwa zikimpigia hesabu beki huyo kijana, jambo lililosababisha katika dirisha kubwa lililopita msimu huu, Simba kukimbilia TFF kushtaki baada ya dili la kumnyakua Lawi kuuliwa na Wagosi walioamua kurudisha sehemu ya fedha iliyomuuza kwa Wekundu hao.
Coastal ilirudisha fedha hizo baada ya Simba kuzitoa kwa mafungu, kinyume cha makubaliano yao na kisha Lawi kwenda KAA Gent ya Ubelgiji ili kutesti nafasi ya kucheza soka la kulipwa kabla ya dili la Ulaya kukwama na kurudia kwa Wagosi na sasa mkataba ukiwa unaenda ukingoni.
Simba ilimkaushia Lawi baada ya kumnasa Abdulrazack Hamza kutoka SuperSports ya Afrika Kusini, kabla ya Yanga kumvizia dirisha dogo, lakini nao walikwama baada ya Coastal kutia ngumu na inaelezwa klabu hizo za Kariakoo, zilikuwa zikimpigia hesabu kumbeba kama mchezaji huru.
Hata hivyo, mabosi wa Coastal wameishtukia janja hiyo na kuamua kumuita mezani beki huyo ili kumshawishi wamuongezee mkataba mpya ili timu zinazommezea mate ziwaache fungu kama zitamsajili kuliko kumuacha aondoke bure.
Taarifa za ndani ya klabu hiyo, zinasema Lawi amefanya mazungumzo ya awali ya kuongeza mkataba mpya ndani ya kikosi hicho kabla ya kwenda AfconU20, japo mabosi wa klabu hiyo wanafanya siri.
Ilielezwa mabosi wa Coastal wamefanya hivyo, baada ya kutambua kuwa Simba na Yanga bado zinampigia hesabu kwa vile zinahitaji beki wa kati, kitu kinachoelewa kwa hatua iliyofikia Lawi mara atakaporudi kutoka Misri atasaini mkataba mpya.
“Mara baada ya mchezaji kurejea kutoka katika jukumu la timu ya taifa, atasaini mkataba mpya kwa vile mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya yalienda vizuri kabla ya kwenda Misri,” kilisema chanzo cha kuaminika ndani ya Coastal.
Mwanaspoti katika kutaka kujiridhisha zaidi iliamua kumtafuta katibu wa timu hiyo, Omary Ayoub ambapo alipoulizwa alisema hayo ni mambo yao ya siri na asingeweza kuyaweka hadharani kwa sasa.
“Lawi kama msimu huu amecheza kwetu inatosha kuona kwamba ni mchezaji wetu. Kuhusu mkataba kuisha hayo ni mambo binafsi ya klabu na mchezaji, hivyo siwezi kuyazungumzia na kama yatakuwapo basi mtapewa taarifa sahihi,” alisema Ayoub.