Kipagwile: Dodoma Jiji hatuna presha

Muktasari:
- Kipagwile aliyetikisa nyavu mara saba na asisti nne msimu huu katika Ligi Kuu akihusika na mabao 11 kati ya 31 yaliyofungwa na timu hiyo, alikiri ameshindwa kufikia malengo ya kufunga mabao kumi, lakini kuihusika katika mabao 11 ni faraja kwake.
WINGA wa Dodoma Jiji, Idd Kipagwile amesema mechi ya mwisho kwa timu hiyo dhidi ya Yanga inayotarajiwa kupigwa Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar haitakuwa na presha kwao kwa sababu tayari wamejihakikishia kubaki Ligi Kuu, japo haina maana watabweteka ili wapigwe.
Kipagwile aliyetikisa nyavu mara saba na asisti nne msimu huu katika Ligi Kuu akihusika na mabao 11 kati ya 31 yaliyofungwa na timu hiyo, alikiri ameshindwa kufikia malengo ya kufunga mabao kumi, lakini kuihusika katika mabao 11 ni faraja kwake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kipagwile alisema wanatambua wanaenda kucheza dhidi ya timu kubwa na watetezi wa taji na ambao hawajawahi kuibuka na ushindi mbele yao, lakini wanaendelea kujiweka tayari na wanaamini wataingia uwanjani bila ya presha kwani tayari wamekata tiketi ya msimu ujao.
“Mchezo wa mwisho kwetu ni wa kukamilisha ratiba hivyo tutaingia bila presha tunaenda kupambana kuhakikisha tunamaliza kwa ushindi licha ya kuwa haitakuwa rahisi kwa sababu tunacheza na timu ambayo inatetea taji lake,” alisema Kipagwile aliyewahi kutamba na KMC na kuongeza;
“Tunaiheshimu Yanga ina wachezaji wengi wazuri lakini sisi pia tunahitaji heshima baada ya mzunguko wa kwanza kupoteza dhidi yao tutapambana kuhakikisha tunagawana pointi mzunguko huu ni wetu tunazihitaji pointi tatu.”
Kipagwile anashika nafasi ya pili kwa ufungaji kikosini Dodoma nyuma ya kinara Paul Peter mwenye mabao manane, alisema huu ni msimu wake bora kutokana na kupata nafasi ya kutupia kambani mabao saba kwani hajawahi kufanya hivyo katika soka la ushindani.
“Mbali na kujipambania kufikia malengo, pia nafurahia kuisaidia timu yangu kubaki Ligi Kuu kwa ajili ya msimu ujao licha ya ushindani mkubwa uliopo. Msimu huu hadi sasa licha ya timu mbili kushuka daraja moja kwa moja bingwa bado hajajulikana na michezo imebaki miwili kwa timu zinazowania taji huku timu nyingine zikibakiza mchezo mmoja.”