Kina Onyango ‘OUT’ CAF

Wednesday April 27 2022
Onyango PIC
By Isiji Dominic

NDOTO ya kuona Wakenya wawili wakinyanyua makombe mawili makubwa Afrika ngazi ya klabu imezimika ghafla baada timu zao kutolewa katika hatua ya robo fainali.

Beki Brian Mandela Onyango alirudi katika kikosi cha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda ya Angola na kuwapatia bao la kuongoza japo mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Pigo kwa Mamelodi ilikua ni kupoteza mchezo wa kwanza ugenini kwa mabao 2-1 mechi ambayo Mandela hakucheza kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa dhidi ya Al Hilal ya Sudan hatua ya makundi.

Sasa nguvu za Mandela na Mamelodi kwa ujumla zimeelekezwa Ligi Kuu ya Afrika Kusini ambapo wanahitaji sare tu mechi ya kesho dhidi ya Cape Town kutwaa taji la tano kwa mpigo itakaowahakikishia kucheza tena Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Mamelodi wamerahisishiwa ubingwa wa Afrika Kusini baada ya wapinzani wao wa karibu, Royal AM kuambulia sare ya kutofungana na AmaZulu huku Kaizer Chiefs wakikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Stellenbosch.

Wakifanikiwa kutetea ubingwa wa Afrika Kusini, Mamelodi watalamba Randi milioni 15 sawa na fedha taslimu za Kenya shilingi milioni 110.

Advertisement

Mbali na kuwa mbioni kutetea ubingwa wa Afrika Kusini, timu ya kina Mandela ipo nusu fainali Kombe la Nedbank na Jumamosi watacheza na Royal AM.

Beki mwingine Joash Onyango akiwa na kikosi cha Simba walipambana lakini wakatolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 na Orlando Pirates ya Afrika Kusini mchezo wa marudiano robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika.

Onyango alikosa mchezo wa kwanza ambayo Simba walishinda bao 1-0 kutokana na kupata kadi tatu za njano na japo alirudi kikosini katika mchezo wa marudiano, Simba walipoteza kwa bao 1-0 na mshindi ikabidi apatikane kwa changamoto za penalti.

Advertisement