Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kikosi cha kwanza cha nyota wa kigeni wanaotesa Ligi Kuu

Muktasari:

Wakati mjadala huo ukiendelea, Mwanaspoti hapa inakuletea kikosi cha wageni 11 bora wanaokinukisha katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu:

MABADILIKO ya kanuni yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya kuruhusu klabu kusajili wachezaji wa kigeni kutoka saba hadi 10, yalipokewa kwa mitazamo tofauti.

Baadhi waliona kuwa mabadiliko hayo yatachangia kuua soka la Tanzania kwa vile klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam ambazo huchangia nyota wengi zaidi katika timu ya Taifa, ndizo zenye nguvu ya kuleta wageni wengi na huenda siku moja mzawa mmoja tu akapata namba kikosini.

Katika mechi yao hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu waliyoshinda 1-0 dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa, Simba walianzisha wazawa watatu tu – kipa Aishi Manula, kiungo Jonas Mkude na straika John Bocco. Wachezaji wanane waliosalia walikuwa ni wa kigeni mabeki Zana Coulibaly (Ivory Coast), Pascal Wawa (Ivory Coast), Juuko Mursheed (Uganda) na Asante Kwasi (Ghana), viungo James Kotei (Ghana) na Clatous Chama (Zambia) na washambuliaji Emmanuel Okwi (Uganda) na Meddie Kagere (Rwanda).

Baadhi ya wadau wanaona kwamba klabu hizo kubwa kutokana na kuhitaji mafanikio kimataifa zinaweza kusajili wachezaji bora 10 na kuacha mzawa mmoja akipata nafasi na hivyo kudhoofisha timu ya taifa.

Wadau baadhi wanaona kwa kuwa klabu hizo kubwa huwavutia wachezaji wenye vipaji kutoka kote nchini na kuwasajili, itakuwa ni hatari kwa soka la taifa pale vipaji hivyo vinapolundikwa katika klabu hizo na kisha kuishia kukaa benchi.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wadau wanaamini kwamba kuwa na wachezaji wengi wa kigeni kutainua soka la Bongo kwani kutawasukuma wachezaji wazawa ambao waliridhika na walipofikia kuanza kupambana ili kuboresha viwango vyao ili kupigania namba dhidi ya wageni.

Wakati mjadala huo ukiendelea, Mwanaspoti hapa inakuletea kikosi cha wageni 11 bora wanaokinukisha katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu:

KIPA:

KLAUS KINDOKI (YANGA)

URAIA: DR Congo

Ni kipa namba moja sasa katika kikosi cha Yanga. Alitua katika kikosi hicho mwanzoni mwa msimu na hakuwa na mwanzo mzuri. Alipotua alikutana na Beno Kakolanya ambaye alikuwa katika ubora wa hali ya juu. Mashabiki hawakuwa na imani naye, walikuwa roho juu kila alipopewa nafasi ya kusimama langoni.

Hata hiyo, sasa amekuwa lulu kikosini baada ya kuokoa penalti mbili za Alliance katika mechi yao ya robo-fainali ya Kombe la FA zilizosaidia kuwapeleka Yanga katika nusu-fainali kuwakabili Lipuli mjini Iringa.

BEKI WA KULIA:

NICHOLAS WADADA

(AZAM FC)

URAIA: Uganda

Azam FC imebahatika kuwa na safu imara ya ulinzi katika miaka ya karibuni na huwezi kuiweka kando ile ya msimu wao pekee 2012-2013 waliotwaa ubingwa bila kupoteza mechi hata moja.

Wameendelea kusajili safu bora ya ulinzi na sasa wanaye beki wa kulia wa timu ya taifa ya Uganda mwenye umri wa miaka 24, Nicholas Wadada.

Azam wamepoteza mechi tatu na wameruhusu magoli 18 katika michezo 30 waliyocheza katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu na wanashika nafasi ya pili katika msimamo.

BEKI WA KUSHOTO:

BRUCE KANGWA

(AZAM FC)

URAIA: Zimbabwe

Licha ya Azam FC kubadilibadili makocha, beki huyu wa kushoto Mzimbabwe mwenye umri wa miaka 31, ameendelea kudumu katika kikosi cha kwanza.

Uwezo wake wa kupanda mbele kusaidia mashambulizi na kushuka haraka katika majukumu yake ya ulinzi, kumewafanya makocha wote wanaokuwa madarakani kumtegemea.

Ni wachache sana wanaofahamu kama nyota huyu wa Azam FC ambaye amekuwa akitumika zaidi kama beki wa pembeni, anaweza kucheza nafasi zote uwanjani isipokuwa kipa.

BEKI WA KATI:

YUSUPH NDIKUMANA (KMC)

URAIA: Burundi

Ni msimu wao wa kwanza KMC kushiriki Ligi Kuu Bara, lakini wameingia katika ligi hiyo wakiwa na moto wa mkali wakionyesha ushindani dhidi ya timu kubwa na nyinginezo, yote ikitokana na kusajili nyota wenye uwezo mkubwa na malengo ya kufika mbali ya hapo walipo. Miongoni mwa nyota waliowasajili na wanafunika kabisa katika ligi msimu huu ni Ndikumana.

Mrundi huyu mwenye umri wa miaka 25 alisajiliwa na KMC akitokea Mbao FC alikocheza kwa kiwango cha juu.

Alihama na kocha wake, Etienne Ndayiragije, ambaye ameonyesha kumuamini akimtumia katika kikosi chake cha kwanza.

BEKI WA KATI:

PASCAL WAWA (SIMBA)

URAIA: Ivory Coast

Aliporejea Tanzania baada ya kuondoka kila mmoja alimbeza kutokana na kushindwa kuonyesha ubora wake kama msimu wake wa kwanza alivyotisha akiwa Azam FC.

Wengi walimponda mara hii alivyotua klabuni Simba wakisema huyu si yule beki kisiki aliyekuwa hapitiki kirahisi na aliyeisaidia Azam kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa ligi msimu wa 2013-14 wakimaliza bila ya kupoteza mechi hata moja.

Wawa mwenye umri wa miaka 33, sasa ni panga pangua katika kikosi cha Simba na amekuwa na msaada mkubwa katika muunganiko wa safu ya ulinzi inayoundwa na Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Erasto Nyoni, ambao kufikia sasa wamepoteza mechi moja tu (dhidi ya Mbao FC) katika mechi 22 za Ligi Kuu ya Bara na wameruhusu magoli machache zaidi ya timu zote.

KIUNGO

STEPHAN KINGUE (AZAM FC)

URAIA: Cameroon

Ni miongoni mwa usajili bora za wachezaji wa kimataifa uliowahi kufanywa na Azam FC, ukiachana na kina Kipre Tchetche ambao waliipa mafanikio makubwa klabu hiyo kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bila ya kupoteza mchezo 2013-14.

Kingue mwenye umri wa miaka 19, amekuwa na mchango mkubwa kwenye klabu ya Azam FC na ni miongoni mwa nyota waliocheza mechi nyingi zaidi kutokana na kuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza.

Kwa kuangalia umri wake mdogo wa miaka 19, Mcameroon huyo ni ‘aseti’ kubwa kwa klabu hiyo pekee inayomiliki uwanja wake wa nyumbani Tanzania.

KIUNGO:

EMMANUEL MVUYEKULE (KMC)

URAIA: Burundi

Kocha Etienne Ndayiragije humwambii kitu kwa mchezaji huyu. Ukimuamsha usiku wa manane akutajie kikosi chake basi jina ya Mvuyekule ni kati majina atakayoyaandika kwanza kwenye karatasi.

Ni kiungo raia wa Burundi aliye katika kiwango chake cha juu kabisa.

Kiwango cha Mvuyekule na nyota wengine wa KMC, vimeiwezesha timu hiyo inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu ya Bara kwanza kushika nafasi ya sita kwenye msimamo wa timu 20, wakiwa na pointi 42 baada ya mechi 32.

KIUNGO

CLATOUS CHAMA (SIMBA)

URAIA: Zambia

Usajili wa kiungo huyu mwenye umri wa miaka 27 klabuni Simba hakika utabaki kuwa historia katika vitabu vya kumbukumbu vya soka la Tanzania.

Pamoja na mambo makubwa anayoyafanya katika Ligi Kuu ya Bara, Chama a.k.a ‘Triple C’ a.k.a Mwamba wa Lusaka, aliibeba Simba mara mbili akiivusha katika hatua kubwa za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Aliifungia Simba bao la ushindi wa jumla ya 4-3 dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia na kuipeleka timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba ililala 2-1 mjini Kitwe katika mechi yao ya awali kabla ya kushinda 3-1 waliporudiana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, shukrani kwa bao tamu la kisigino la Chama katika dakika ya 88.

Chama pia aliifungia Simba goli la dakika za lalasalama la ushindi wa 2-1 dhidi ya AS Vita katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwapeleka Wekundu wa Msimbazi robo fainali.

STRAIKA

MEDDIE KAGERE (SIMBA)

URAIA: Rwanda

Ukitaka kugombana na mashabiki wa Simba toa maneno ya kumkejeli MK14.

Kagere, mwenye umri wa miaka 32, ameingia kwa kishindo Simba. Ndiye mchezaji anayeongoza kikosini mwao hivi sasa kwa kufunga magoli mengi katika Ligi Kuu ya Bara akitupia mabao 14 baada ya mechi 22 kufikia sasa.

Aliisaidia Simba kufika robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akifunga magoli sita na ni kama mchezaji ambaye unaweza kusema amekuja kuzima kabisa ufalme wa Okwi Msimbazi.

STRAIKA

EMMANUEL OKWI (SIMBA)

URAIA: Uganda

Ni mshambuliaji mwenye kipaji kutoka Uganda ambaye kwa miaka mingi amekuwa ndiye kipenzi cha mashabiki wa timu ya Simba.

Alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopita alipotupia mabao 20 na msimu huu ameendelea kuwa silaha muhimu ya kocha Mbelgiji Patrick Aussems akutupia mabao saba.

Straika huyo mwenye umri wa miaka 26, ndiye aliyefunga goli pekee lililokuwa la kuongoza la Simba katika mechi yao ya marudiano ya robo faibali ya Ligi ya Mabingwa Afrika waliyolala 4-1 dhidi ya TP Mazembe mjini Lubumbashi Jumamosi iliyopita.

STRAIKA

HERITIER MAKAMBO (YANGA)

URAIA: DR Congo

Heritier Ma Olongi Makambo yuko katika kiwango chake bora klabuni Yanga licha ya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Bara kuwa katika mtikisiko mkubwa wa kiuchumi.

Matatizo ya mishahara na mengine yanayoitafuna klabu hiyo ya Jangwani, hayajamzuia straika huyu mrefu mwenye umri wa miaka 25 anayetumia mguu wa kushoto kuendelea kuwanyoosha makipa wa upinzani kwenye Ligi Kuu na michuano mingine ikiwamo Kombe la FA.

Anakimbizana kileleni mwa msimamo wa vinara wa ufungaji msimu huu wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 15, moja tu nyuma ya mzawa Salum Aiyee wa Mwadui anayeongoza kwa kufunga mabao 16.

KOCHA

MWINYI ZAHERA (YANGA)

URAIA: DR Congo

Licha ya kuongoza timu yenye mdororo wa kiuchumi unaosababisha mara kadhaa wachezaji kugoma kufuatana na kikosi kwenye baadhi ya mechi, Zahera ameiwezesha Yanga kubaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Bara.

Ameiwezesha kutinga nusu-fainali ya Kombe la FA ambako itakutana na Lipuli mjini Iringa na pia amevunja mwiko wa timu hiyo kushindwa kupata ushindi katika uwanja wa CCM Kirumba kwa kuzifunga timu za Mbao FC na Alliance.

WACHEZAJI WA AKIBA

Kipa: Razack Abalora

(Azam, Ghana).

Mabeki: Zana Coulibaly (Simba, Ivory Coast), Juuko Mursheed (Simba, Uganda).

Viungo: James Kotei (Simba, Ghana), Papy Tshishimbi (Yanga, DR Congo)

Washambuliaji: Obrey Chirwa (Azam, Zambia), Donald Ngoma (Azam, Zimbabwe).