KIBANDA UMIZA: Kisa kufungwa Simba, mwenye banda azima TV

ACHA kabisa kufungwa kunauma. Hii ilikuwa ni michongo ya kizamani kidogo, lakini timu ya kibanda umiza ilifanikiwa kulipata tukio hilo wiki iliyopita kwenye mechi ya Simba dhidi ya Yanga iliyopigwa jijini Mwanza.

Kwenye banda lililopewa jina la Watuku Arena maeneo ya Kizuiani, Temeke - Dar es salaam lilitokea tukio hilo baada ya Yanga kufanikiwa kupata bao la kwanza lililofungwa na Feisal Salum, kuliibuka kibweka cha aina yake kutoka kwa mwenye banda. Muda mfupi baada ya bao kuingia wakati watu wakiendelea kushangilia mwenye banda hilo ambaye ni shabiki wa Simba alitoka bandani huku mkononi akiwa ameshika rimoti.

Alipotoka tu na televisheni ikazima na kuacha watu kwenye taharuki, baadhi yao wakishtuka na kusema kwamba jamaa ndiye aliyezima. Baadhi ya watu walimfuata na kumwambia kwamba televisheni ilikuwa imezima, lakini alipoingia bandani aliwaambia ni tatizo la kiufundi.

“Wewe umezimaaa... sasa kama hutaki tuangalie si useme tu sisi tumelipa hela hapa..”

Mwenye banda akajibu: “Sasa kama umelipa hela si ukalipe sehemu nyingine ukaangalie..” Ilichukua muda mfupi kwa malumbano hayo kabla ya jamaa kushikashika nyaya na baadaye kubonyesha kitufe kwenye rimoti na tv ikawaka watu wakaendelea kuangalia kama kawaida.

Baada ya mpira kwisha yule jamaa mwenye banda wakati anabishanabishana na wenzake alikiri kweli kwamba alizima tv kwa kuumizwa na matokeo.


Je!! Huko kuna vaibu kama lote? Basi tupe mwaliko kupitia namba 0713-085905 au 0734-035599 ili wazee wa vibanda umiza, Eliya na Mtupa tuje kuliamsha