Kaze: Tunakuja kivingine

Sunday February 28 2021
kazee pic
By Oliver Albert

MASHABIKI wa Yanga licha ya kuchekelea timu yao ikitinga 16 Bora baada ya jana kuifunga Ken Gold ya Daraja la Kwanza kwa bao 1-0 katika mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC), ila bado wanaonekana kutoridhishwa na kiwango cha baadhi ya nyota wao, lakini kocha wao, Cedric Kaze amewatuliza akiwaambia wasihofu kwani, mambo matamu yanakuja.

Yanga ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kwa bao la mkwaju wa penalti kupitia mshambuliaji wao mpya, Fiston Abdulrazack, lililokuwa la kwanza kwake katika mechi za mashindano tangu asajiliwa mapema mwezi uliopita.

yanga full pic

Penalti hiyo ilipatikana dakika ya 42 baada ya Boniface Mwanjonde kuunawa mpira katika harakati za kuokoa na mwamuzi Ahmed Ajariga kutoka Manyara kutoa adhabu hiyo na Fiston kupiga kiufundi kuiandika Yanga bao pekee kwenye mchezo huo uliokuwa mkali.

Ushindi huo umeifanya Yanga kuungana na watani wao, Simba kutinga hatua ya 16 Bora, lakini baadhi ya mashabiki waliohudhuria mchezo huo wamesikika wakilalamikia umakini mdogo wa nyota wa kikosi chao kilichowafanya washindwe kutokana na kapu la mabao mbele ya Ken Gold.

Hata Kocha Kaze naye aliliona jambo hilo na kukiri anajipanga na kubadilisha mbinu zake ili mambo yawe matamu zaidi Jangwani katika mechi zao zijazo ikiwamo ile ya Alhamisi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Advertisement

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kaze alikiri haukuwa mchezo rahisi kwao kwa madai ya hali ya hewa haikuwa nzuri na pia uwanja ulikuwa mgumu huku akidai majeruhi wengi katika kikosi chake kimeigharimu timu, lakini anawatoa hofu wanayanga.

“Tumemiliki mpira sana, lakini hatukuwa wepesi wakati tupo katika eneo la mwisho ili kupata mabao mengi. Lakini muhimu ni tumefuzu kwenda hatua nyingine. Kutokuwa na upana wa kikosi nalo ni tatizo kwani wachezaji wakiumia wale wanaochukua nafasi hata kama hawaonyeshi kile unachotarajia unashindwa kufanya,” alisema Kaze na kuongeza;

“Ninachofurahi wachezaji wote majeruhi wameanza kurudi katika hali zao za kawaida naamini mechi zijazo, tutakuwa vizuri zaidi na hasa kwenye mchezo wetu dhidi ya Coastal Union.”

Kaze aliongeza mchezo huo wa Tanga utakaopigwa Alhamisi hautakuwa rahisi, lakini wanaenda kujipanga ili kuhakikisha tunapata ushindi ili kuendeleza rekodi yao na kuwaomba, mashabiki waendelee kuisapoti timu yao kwa mechi hiyo ya Tanga na nyinginezo.

Katika mchezo huo wa jana uliochezwa vyema na mwamuzi Ajariga, nyota wa Yanga wakiongozwa na Fiston, Ditram Nchimbi, Deus Kaseke na Farid Mussa waliounda safu ya ushambuliaji walitengeneza nafasi nyingi, lakini wakazipoteza.

Katika kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Deus Kaseke na Nchimbi na kuwaingiza Carlos Carinhos na Haruna Niyonzima mabadiliko yaliyoichangamsha kidogo Yanga kipindi cha pili kwani dakika moja tu tangu Carlinhos aingioe alikosa bao la wazi baada ya mpira wake wa kichwa akimalizia krosi ya Farid kudakwa na kipa Adam John aliyekuwa makini.

Hata hivyo Carlinhos alidumu uwanjani kwa dakika 16 kabla ya kutolewa uwanjani kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga ngumi ya kiuno Boniface Mwanjonde kutokana na kukerwa na alivyomdhibiti kwa kumsukuma kwa mikono nje ya uwanja.

Katika mchezo huo kama kuna mchezaji aliyepata wakati mgumu basi ni Nchimbi ambaye ana muda mrefu hajafunga bao na jana mashabiki walikuwa wakimzomea kila alipofanya makosa na kelele zao huenda ndizo zilizomfanya Kaze ampumzishe dakika ya 66 kumwingiza Carlinhos aliyeshangiliwa kabla ya kuzingua na kuiachia timu yake pengo uwanjani.

Kocha wa Ken Gold, Salvatory Edward aliwasifia vijana wake kwa mchezo mzuri na kuwabana Yanga kwa muda mrefu, licha ya kuangushwa na uzoefu na kutojiamini mbele ya nyota wa Yanga.

Advertisement