Ajibu amvuruga Gomes

Sunday February 28 2021
ajibu pic
By Thobias Sebastian

SOKA tamu lililojaa ufundi na umakini, lililopigwa na kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu limemvuruga kocha wake, Didier Gomes, huku nyota huyo akisisitiza akizidi kupewa nafasi kikosini atafanya mambo makubwa zaidi kuliko alichokifanya kwenye Kombe ASFC.

Wekundu wa Msimbazi hao juzi walishinda mabao 3-0 dhidi ya African Lyon na kutinga 16 Bora ya michuano hiyo ya ASFC, huku Ajibu akitupia mbili nyavuni na jingine likiwekwa kimiani na Perfect Chikwende na Kocha Gomes amemsifia sana Ajibu akidai ni bonge la fundi.

Akizungumza na Mwanaspoti juzi jijini Dar es Salaam, Gomes alisema Ajibu ameonyesha kiwango bora katika mechi hiyo ya ASFC na kwamba anaongeza ushindani zaidi wa namba kwenye nafasi anayocheza ili aingie kikosi cha kwanza alichodai pia kina wachezaji wengine wakali kama yeye.

Gomes alisema hana utamaduni wa kusifia mchezaji mmoja mmoja, lakini alichokifanya Ajibu kimemkuna kama alivyokuna na soka la wengine aliowaanzisha kwenye mchezo huo hasa wale wasiopata nafasi katika kikosi cha kwanza.

“Ajibu ni mchezaji mzuri mwenye uwezo wa kumiliki mpira, jicho la kupiga pasi yenye hatari, kufunga mabao pamoja na mambo mengine na alistahili kuonyesha kiwango hicho kwa vile alikuwa akikifanya hata mazoezini,” alisema Gomes na kuongeza;

“Niwapongeze wachezaji wangu hawakuonyesha utofauti mkubwa licha ya kubadilisha kikosi hii inaonyesha jinsi gani nao wanataka kupewa nafasi ya kutumika zaidi kwani wana viwango bora na malengo yetu ni kutetea kombe hili.”

Advertisement

Gomes alisema pia wao kila mechi wanaichukua kwa uzito wake kama ilivyokuwa katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika wakijiandaa kuvaana na maafande wa JKT Tanzania mechi itakayopigwa kesho jijini Dar es Salam kabla ya Jumanne kusafiri kuwafuata El Merreikh ya Sudan.

Simba imepangwa Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kwa sasa ni kinara wa kundi hilo wakiwa na alama sita baada ya kupata ushindi wa mechi zao mbili za awali dhidi ya As Vita ya DR Congo na Al Ahly ya Misri na mechi yao ya tatu itapigwa Ijumaa mjini Odurman dhidi ya Wasudan hao.


MSIKIE AJIBU

Kwa upande wa Ajibu alisema mara zote huwa katika kiwango bora ila suala la kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, linabaki kuwa jukumu la kocha wake.

“Nimekuwa nikicheza mara zote, nimecheza wakati huu na nitaendelea kufanya hivi hivi katika mechi nitakazopewa nafasi ya kucheza kwa mara nyingine binafsi najiamini nipo vizuri katika kutimiza majukumu yangu uwanjani,” alisema Ajibu mwenye bao moja la Ligi Kuu na kuongeza;

“Simba ina wachezaji wengi wazuri na huenda wanaopewa nafasi ya kucheza badala yangu wapo bora zaidi, ila hilo si kitu kwangu naendelea kupambana na kujiandaa vizuri ili nitakapopata nafasi nyingine nionyeshe ubora zaidi.”

Advertisement