Vigogo Afrika kupambana kwa Mkapa

Waalgeria, Mamelodi kuchezwa bila mashabiki kwa Mkapa

LEO Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar se Salaam saa 10:00 jioni kutachezwa mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kati ya CR Beluoizdad ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Sababu kubwa ya mchezo huo kuchezwa nchini ni kutokana na CR Beluoizdad kuomba mechi yake ya nyumbani ichezwe hapa badala ya nchini kwao Algeria ambako bado kuna changamoto ya maambukizi ya virusi vya corona.

Pamoja na mechi hiyo kuchezwa nchini lakini Watanzania hawatapata fursa ya kuingia uwanjani kuzishuhudia timu hizo kwani CR Beluoizdad ambao ni wenyeji kutoruhusu mashabiki kuingia uwanjani hivyo mtanannge huo utapigwa bila mashabiki.

Awali gazeti la Mwanaspoti liliwanasa baadhi ya viongozi wa juu wa Mamelodi wakizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Simba Barbara Gonzalez wakiomba sapoti ya mashabiki wao kuwashangilia kwenye mchezo huo jambo ambalo limeshindikana baada ya CR Beluoizdad kukataza mashabiki katika mechi hiyo.

Mamelodi ni vinara wa kundi B lenye timu za TP Mazembe, Al Hilal na CR Beluoizdad wakiwa na alama tatu walizopata kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal waliposhinda 2-0 wataingia uwanjani wakihitaji alama tatu muhimu ili kuzidi kuongoza kundi hilo huku Beluoizdad nao wakihitaji ushindi utakaowapeleka kileleni mwa kundi hilo kwani mpaka sasa wapo nafasi ya tatu wakiwa wamecheza mechi moja dhidi ya TP Mazembe iliyomalizika kwa sare.

Mamelodi wamewahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka 2016 na mabingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini mara 10 huku CR Belouizdad wakibeba mara saba kombe la Ligi kuu ya Algeria.