Kaze azipa nafasi timu nne Ligi Kuu

Dar es Salaam. Kocha mkuu wa mabingwa wa kihistoria, Cedric Kaze amesema hakuna timu yenye dhamana na ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Kaze, ambaye tangu ametua Yanga Oktoba mwaka jana ana rekodi ya kutopoteza mechi kwenye Ligi Kuu na amezipa nafasi ya ubingwa timu nne.
Pamoja na kwamba Yanga ipo kileleni kwenye msimamo na sare ya juzi ya Simba na Azam imeendelea kuwabeba katika harakati za ubingwa, Kaze alisema bado hawana dhamana ya kujihakikishia ubingwa.
“Tuna mechi 16 ili kumaliza msimu, katika mechi hizo tunatafuta pointi 48, hizi ni pointi nyingi sana katika ligi yenye ushindani, si kwa Yanga tu, hata Simba ambayo tunachuana nayo kwa karibu,” alisema Kaze.
Alisema timu kama Azam na Biashara pia zina nafasi ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubingwa japo mashabiki wanaona zina pointi chache kulinganisha na za Simba au Yanga.
Biashara ni ya nne ikiwa na pointi 29 na Azam ina pointi 33, ikiwa ya tatu katika msimamo zote zina mechi 16 mkononi za kucheza.