Kaze atua na yake

MCHANA wa jana Kocha Mkuu mpya wa Yanga, Cedric Kaze alitarajiwa kuianza safari kutoka Canada kuja Tanzania kujiunga na timu hiyo, huku ikielezwa ametoa maelekezo kwa mabosi wa klabu hiyo kutaka wachezaji wakafichwe kambi ya Kigamboni wakijifua na kulala huko huko.

Kocha huyo anatarajiwa kutua usiku wa leo kwa ndege ya KLM kabla ya asubuhi ya kesho kujumuika na vijana wake kwenye mazoezi baada ya kufanyiwa utambulisho kwa wachezaji hao na watu wa benchi la ufundi.

Awali, Kaze alilidokeza Mwaanspoti alikuwa atue nchini Jumatano, kabla ya kufafanua hiyo jana ndio safari yake ilikuwa ianze kisha ndipo awasili leo ili kuanza kazi akichukua nafasi ya Zlatko Krmpotic aliyefurushwa baada ya kuiongoza timu kwenye mechi tano za Ligi Kuu Bara na kushinda nne.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, kocha huyo alikuwa ameanza safari yake na ametaka wachezaji wasifanye mazoezi Chuo cha Sheria wakitokea majumbani kama ilivyo sasa badala yake waweke kambi ya kudumu ili awalishe madini, kwa mechi nne za ligi kabla ya kuvaana na watani wao.

Yanga itacheza mechi nne dhidi ya Polisi Tanzania itakayopigwa Jumatano ijayo, KMC, Biashara United na Gwambina ikiwa ugenini kabla ya kurejea kuvaana na Simba Novemba 7 likiwa pambano lao la kwanza msimu huu na la 105 klatika ligi ya Bara tangu 1965.

Mwanaspoti ilijaribu kuwasiliana na kocha huyo ili kujua ishu yake ya safari na juu ya ujio wake usiku wa leo, lakini hakuweza kupatikana hewani, licha ya kupokea ujumbe mfupi kwa njia wa WhatsApp.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla alipotafutwa kwa njia ya simu jana ili kufafanua juu ya ujio wa kocha huyo Mrundi, simu yake iliita bila kupokewa.