Karia aipongeza Simba akizitaka klabu zingine ziige

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefurahishwa na namna ambavyo klabu ya Simba imejipapatua mpaka kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba imetinga hatua hiyo baada ya kumaliza katika kundi lao ikiwa na pointi 13 akifuatiwa na Al Ahly akiwa na pointi 11 huku Al Merrikh na As Vita wakikosa nafasi ya kufuzu ndani ya kundi hilo.

Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia ameiambia Mwanaspoti Online kuwa, kama TFF wanajivunia mafanikio ya Simba ambayo yanazidi kulitangaza soka la Tanzania.

Amesema, Simba inahitaji pongezi na timu nyingine zinatakiwa kuiga mazuri yaliyofanywa na Simba mpaka kufikia hatua hiyo ambayo kila Mtanzania anatakiwa kujivunia mafanikio hayo.

"Simba nawapongeza sana, kwa namna ambavyo wamepambana mpaka kufikia hatua waliyofikia, nawaombea wazidi kufanya vizuri na kuweka historia ya kulitwaa taji hilo, kufanya kwao vizuri ni heshima kubwa Tanzania inazidi kujulikana zaidi na zaidi,"amesema.

Karia amesema, licha ya Namungo kutofanya vizuri katika michezo yaker ya makundi lakini anaipongeza kutokana na uchanga wao na namna ambavyo wamepigana kufikia walipofikia mpaka sasa.

"Namungo wamepambana sana sana, na hata katika uwakilishi wa timu nne hata wao wamechangia kwa kiasi fulani hivyo nawapongeza sana na wao,"amesema Karia.

Droo ya hatua hiyo inatarajiwa kuchezeshwa April 30 huku mechi zake zikitarajiwa kupigwa Mei 14-15 mwaka huu.