Kagera Sugar sasa yatoa ahadi
LICHA ya kuanza kwa kasi ya chini katika mechi nne za Ligi Kuu, benchi la ufundi la Kagera Sugar limewatoa wasiwasi mashabiki wake na kuwaahidi kuwa bado kidogo tu timu yao iwe kwenye ubora wanaoutegemea kwani wanapambana kuhakikisha inafanya vizuri na kumaliza tatizo linalowasumbua la kufunga mabao.
Timu hiyo ambayo kesho Oktoba 4 itakuwa nyumbani kucheza na Namungo saa 1 jioni katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba huku ikishusha kiingilio mpaka Sh1,000 mzunguko na Sh3,000 jukwaa kuu, imevuna pointi nne katika mechi nne ikipoteza mbili, sare moja na kushinda moja.
Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Chamberi Marwa amesema kuanza kwa mwendo usioridhisha haimaanishi kwamba kikosi chao ni kibovu bali kila mchezo kwa sasa wanauchukulia kama fainali na benchi linapambana kurekebisha makosa yaliyopo.
Kuhusu changamoto ya ufungaji mabao ambapo timu hiyo imefunga mabao mawili pekee katika mechi nne, Marwa alisema kwamba kila siku mazoezini wamekuwa na programu ya kutengeneza nafasi na kufunga mabao lakini uwanjani kwenye mechi mambo yanakwenda tofauti.
“Tulianza ligi kwa mwendo usioridhisha lakini haimaanishi kwamba sisi ni wabovu, mpaka hapa tulipofika kila mechi tunaichukulia kwa umuhimu na kama fainali tuweze kupata ushindi hata kwa mechi zinazokuja tunaendelea kupanda taratibu mpaka tupate ubora wetu ambao tunautarajia msimu huu,” alisema Marwa.
“Lakini polepole nina imani kwa sababu nafasi tunatengeneza umaliziaji ndiyo unakuwa shida kwahiyo kama tunatengeneza nafasi za kufunga inamaana imebaki sehemu ndogo ya kuweza kufunga kwahiyo tunalifanyia kazi hatutachoka mpaka pale tutakapopata magoli ya kutosha.
“Mchezo ujao ni tofauti na JKT kwa hiyo maandalizi yetu yatakuwa tofauti tutaenda kukaa chini tunajua wanavyocheza na tuwakabili vipi tumeangalia mechi zao kwa hiyo tumejiandaa kuhakikisha tunapata pointi tatu nyumbani,”
Nyota wa timu hiyo, Gasper Mwaipasi aliyefunga bao katika mchezo uliopita, alisema “Mashabiki ni watu muhimu sana kwahiyo tunawahitaji waje kwa wingi timu yao wanatakiwa waisapoti kwa hali na mali, mpira una misukosuko mingi kwahiyo inabidi wasichoke wawe na sisi katika nyakati zote na waje kwa wingi katika mchezo huu.”