JIWE LA SIKU: Tatizo ni hawa kina Pacome, Waamuzi

Muktasari:

  • Klabu zenye ushawishi kwa mashabiki uwanjani, Simba na Yanga zimo kwenye 10 bora. Kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mara mbili miaka ya karibuni pia sio kwa bahati mbaya. Kuna namna tunapiga hatua kubwa sana kwenda mbele.

Ligi Kuu Bara kwa sasa inatajwa kwenye tafiti mbalimbali za nje ya nchi. Si bahati mbaya. Kuna kitu kimeongezeka.Moja ya tafiti hizo, ni ya ligi zinazotengeneza pesa nyingi Afrika. Tanzania iko ndani ya 10 bora. 

Klabu zenye ushawishi kwa mashabiki uwanjani, Simba na Yanga zimo kwenye 10 bora. Kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mara mbili miaka ya karibuni pia sio kwa bahati mbaya. Kuna namna tunapiga hatua kubwa sana kwenda mbele.


Baada ya miaka mingi kupita, Simba na Yanga kwa sasa zipo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Sio jambo dogo. Kuna mahali tunaelekea. Zama za timu kutoka Tanzania kwenda kupigwa mabao mengi na timu za Kaskazini mwa Afrika, nazo zimekwisha. 


Taifa Stars haikufanya vizuri kwenye Fainali za Afcon 2023, zilizomalizika hivi karibuni Ivory Coast, hata hivyo,  kuna namna ubora umeongezeka. 


Tulipangwa kundi moja na Morocco, Zambia na DR Congo, wote wameshabeba taji la Afcon isipokuwa Tanzania. Sare dhidi ya Zambia na DR Congo ni ishara nyingine tumeongezeka ubora. 
Kitendo cha Yanga kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, ni dalili njema taji la Afrika liko mbioni kuja Tanzania.


Kwa upande wa Taifa Stars, nadhani njia kuu ni moja tu. Ni ngumu sana kupata ubingwa wa Afrika kwa kutegemea wachezaji wanaocheza Afrika. 


Afrika Kusini ni miongoni mwa Ligi inayolipa mishahara mizuri namba mbili Afrika. Afrika Kusini ni moja ya mataifa yenye miundombinu bora ya michezo Afrika, lakini bado ni ngumu kwao kutamba Afcon. Kushinda Afcon kunahitaji uwekezaji mkubwa sana nje ya Afrika.


 Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, TFF na klabu, wanahitaji kufanya kikao cha pamoja. Kwa nchi kama yetu, tunahitaji msaaada wa Serikali kupeleka vijana nje kimkakati. 


Kwenye balozi zetu, ni rahisi kuweka mkakati wa kupeleka vijana wengi nje ili baada ya miaka 10, tuwe na kijiji cha kutosha kutoka Sweden, Ubelgiji, Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya. 


Wachezaji kama Clement Mzize, Abdul Soup, Ladaki Chasambi, Abdultwalib Mshery ndiyo Taifa Stars ya kesho. Kwa nchi yetu, ni muhimu kuwa na mkakati wa kivyetu vyetu.


 Hawa vijana wanatakiwa kusimamiwa na nchi. Tukisema tunawaachia wachezaji wenyewe, bado kutakuwa na ugumu. Ni lazima uwe ni mpango wa nchi kupeleka vijana Ulaya. 


Klabu peke yake hasa za Simba na Yanga, haziwezi kukubali peke yao. Maana na wao wanahitaji kushindana hapa ndani. Ukiwekwa mkakati wa pamoja wa kupeleka vijana nje kwa msaada wa balozi zetu, baada ya muda tutakuwa na wachezaji wazuri. Ni muda sasa wa kujiongeza. Taji la Afrika linataka mipango madhubuti.


Klabu zetu zinaongezeka ubora msimu kwa msimu. Ni muda sasa wa kuleta taji la Afrika nyumbani. Zamani kucheza robo fainali ya michuano ya Afrika ilikuwa inakuja kama bahati lakini kwa sasa sio mafanikio tena. Kuna uwekezaji mkubwa wa wachezaji na makocha unafanywa Tanzania. Simba, Yanga na Azam FC zimepiga hatua kubwa sana. 


Naona Singida Fountain Gate, Tabora United na Namungo FC nao wanafuata nyayo. Naanza kuona dalili za ubingwa wa Afrika siku moja kuja Tanzania. 


Simba na Yanga zimeboresha bajeti zao hasa kwenye kuwaleta wachezaji wa kigeni na kina Pacome Zouzoua na Clatous Chama ni bora zaidi kwenye ligi yetu, muda si mrefu tutapokea kombe pale Terminal 3.


Tumekuwa na wachezaji wengi sana kwenye Afcon hii wanaocheza Tanzania kuliko kipindi kingine chochote. Djigui Diarra, Henock Inonga, Aziz KI, Chama ni sehemu tu ya nyota kutoka ligi ya Tanzania.


 Miaka ya nyuma, hali ilikuwa tofauti. Wachezaji wengi hasa wa kigeni waliocheza Tanzania hakuwa wanaitwa kwenye mataifa yao. Kuna mahali tumesogea. Kumekuwa na sajili nzuri Simba, Yanga na Azam FC. Tunaelekea kuzuri. Naanza kuona dalili za Kombe la Afrika kuja Tanzania. Soka letu pamoja na changamoto zake, linakua kwa kasi.


Eneo dume ambalo bado hatujatoboa ni waamuzi. Tuna waamuzi ambao walipata nafasi ya kuitumikia Caf, hata hivyo hatuna cha kujivunia.


 Suala la waamuzi bado ni tatizo kubwa. Ni kama kila siku tunazidi kupiga hatua nyingi kurudi nyuma. Nadhani eneo hili tunahitaji kuwekeza nguvu kubwa sana. 


Fainali za Afcon zimemalizika. Tanzania haikuwa na mwamozi hata mmoja. Sio bahati mbaya. Viwango vyao ni vichekesho vitupu.


Kila wikendi ukitazama ligi yetu, huwezi kukosa kituko cha mwamuzi. Simba, Yanga na Azam pamoja na uwezo wao, lakini wamekuwa wanufaika wakubwa wa madudu ya waamuzi wetu.
 Ubingwa wa Afrika ni ngumu kuupata kama wachezaji wetu wanachezeshwa na waamuzi wabovu ambao huleta matokeo mabovu! 


Hakuna namna hili eneo nalo linahitaji uwekezaji mkubwa.
Waamuzi wetu wanahitaji kujengewa uwezo. Bado tunahitaji pia kutengeneza makocha wetu wazawa. 


Rwanda, Kenya na Burundi wamekuwa na makocha wengi wanaokuja kufanya kazi Tanzania. Makocha wetu wengi ni wa hapa hapa. Hakuna anayetoka na wengi wanaridhika kuwa makocha wasaidizi kwa wageni.


 Nadhani tunahitaji pia kubadilika hapa. Matatizo mengi tunayopitia Taifa Stars wakati mwingine yanaletwa na makocha wa kigeni. 


Sina tatizo na kocha wa kigeni kufundisha Taifa Stars, lakini tukipata mzawa itakuwa nzuri zaidi. Uzalendo kwenye timu ya Taifa unaletwa na kocha mzawa.